1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal yatangaza kuandaa uchaguzi haraka iwezekanavyo

17 Februari 2024

Serikali ya Senegal imetangaza kuwa uchaguzi wa rais ulioahirishwa utafanyika haraka iwezekanavyo, siku moja baada ya Baraza la Katiba la nchi hiyo kubatilisha amri ya rais Macky Sall ya kuusogeza mbele kwa miezi kadhaa.

https://p.dw.com/p/4cWBt
Senegal, Dakar | Rais Macky Sall
Rais wa Senegal Macky SallPicha: Sylvain Cherkaoui/AP/picture alliance

Msemaji wa Rais Sally, Yoro Dia, amesema kuwa rais anakusudia kutii maamuzi hayo ya Baraza la Katiba ambalo lilisema hapo jana kuwa kuuchelewesha uchaguzi huo uliopangwa mnamo Februari 25 hadi Desemba 15, ni kinyume na katiba. Hata hivyo msemaji huyo hakutaja tarehe mpya ya uchaguzi.

Soma pia:Serikali ya Senegal yasaka suluhu ya mzozo wa kuahirisha uchaguzi

Senegal ilichukuliwa kuwa mojawapo ya nchi zenye demokrasia thabiti katika eneo la Afrika magharibi ambalo limeshuhudia mkururo wa mapinduzi ya kijeshi, lakini misuguano kuhusu uchaguzi wa mwaka huu imelitumbukiza taifa hilo kwenye mzozo wa kisiasa, ikiwemo kufanyika maandamano ya ghasia yaliosababisha vifo vya watu watatu na wengine kadhaa wakiwemo maafisa usalama kujeruhiwa.