1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal yasaka suluhu mzozo wa kuahirisha uchaguzi

16 Februari 2024

Serikali ya Senegal imesema mirengo ya kisiasa nchini humo inahitaji kushauriana na kutafuta njia ya kusonga mbele baada ya Baraza la Katiba kutoa uamuzi kwamba kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais ni kinyume cha sheria.

https://p.dw.com/p/4cUWG
Rais Macky Sall wa Senegal.
Rais Macky Sall wa Senegal.Picha: Amr Alfiky/File Photo/REUTERS

Akizungumza kwenye mahojiano na redio moja ya kibinafsi nchini humo siku ya Ijumaa (Februari 16), msemaji wa serikali, Abdou Karim Fofana, alisema kwamba serikali imezingatia uamuzi wa Baraza la Katiba, lakini hakufafanua ikiwa hilo linaamisha kwamba ingelikubali maamuzi hayo.

Ofisi ya Rais pia haikusema lolote kuhusu iwapo ingeliuheshimu uamuzi huo.

Soma zaidi: Wabunge wakamatwa wakipinga kuahirishwa uchaguzi Senegal

Wakati huo huo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imetoa wito kwa mamlaka nchini Senegal kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi wa rais kulingana na uamuzi huo wa Baraza la Katiba, ambao ulisema kuahirishwa kwake kulikuwa kinyume cha katiba.

Umoja wa Ulaya pia umezitaka pande husika nchini Senegal kutii uamuzi huo wa Baraza la Katiba.