1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz, Biden waahidi kuendelea kuisaidia Ukraine

Grace Kabogo
4 Machi 2023

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz na Rais wa Marekani Joe Biden, wameapa kuendeleza ushirikiano wao wa pamoja kuisaidia Ukraine.

https://p.dw.com/p/4OFNq
Weißes Haus Treffen Scholz und Biden
Picha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Matamshi hayo wameyatoa siku ya Ijumaa wakati Scholz alipokutana na Biden katika Ikulu ya Marekani, White House. Viongozi hao wamekutana huku kukiwa na wasiwasi kwamba China ianweza kuanza kupeleka silaha za kivita nchini Urusi.

Scholz na Biden wamezungumzia umoja wao na wameelezea dhamira yao ya kuiunga mkono Ukraine, kutokana na mvutano wa hivi karibuni kuhusu kuipatia Ukraine vifaru. Scholz amesema ushirikiano na Marekani uko katika hatua nzuri na muhimu kwamba wamechukua hatua pamoja na kwamba mara kadhaa anaamini kuwa serikali yake inahitaji kuwa katika ushirikiano na utawala wa Biden.

Soma zaidi: Scholz awasili Marekani

Biden amemshukuru Scholz kwa uongozi wake imara na thabiti ambao umeleta mabadiliko makubwa. Biden pia amempongeza Scholz kwa uamuzi wake wa kuongeza matumizi ya jeshi la Ujerumani na kubadilisha vyanzo vya nishati na kupunguza kutegemea gesi ya Urusi. ''Kama washirika wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, tunaufanya muungano huu wa kijeshi kuwa na nguvu,'' alifafanua Biden.

Viongozi hao walifanya mazungumzo katika kikao cha faragha, lakini pia walizungumza kwa muda mfupi mbele ya waandishi habari. Hii ni ziara ya kwanza ya Scholz nchini Marekani, tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine, Februari 24, 2022.

Kwa nini Marekani na Ujerumani wana wasiwasi kuhusu China?

Kabla ya mkutano huo, kansela huyo wa Ujerumani aliitolea wito China kutumia ushawishi wake kuishinikiza Urusi kuyaondoa majeshi yake na sio kusambaza silaha kwa Urusi. Scholz aliutoa wito huo siku ya Alhamisi katika hotuba yake kwa Bunge la Ujerumani.

Russland Moskau | Wladimir Putin und Wang Yi
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa China, Wang Yi na Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: Anton Novoderezhkin/ITAR-TASS/IMAGO

Msemaji wa baraza la usalama la Marekani John Kirby, ameiambia DW kwamba bado hawajapata dalili zozote kama China imeamua kusonga mbele kuipatia Urusi aina yoyote ya silaha. ''Hawajaliondoa suala hilo mezani, lakini hatuna ishara yoyote ambayo inaonesha wanaelekea upande huo kwa sasa, na kwa hakika tuna matumaini kwamba ahwatofanya hivyo,'' alisisitiza Kirby.

Hatua kama hiyo inaweza kusababisha msuguano kati ya Ujerumani na Marekani kutokana na misimamo yao tofauti kuhusu China. Nchi hiyo ya Asia ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Ujerumani, na uwezekano wa Marekani kuiwekea vikwazo China iwapo itaamua kupeleka silaha, unaweza kusababisha matatizo kwa Berlin ambayo inasema Beijing inaweza kuwa na jukumu katika kuleta amani.

Muda mfupi kabla ya mkutano wa Biden na Scholz, Urusi iliyaonya mataifa ya Magharibi dhidi ya kutoa silaha zaidi kwa Ukraine. Lakini Marekani imetangaza msaada mpya wa dola milioni 400 kwa ajili ya msaada wa usalama nchini Ukraine.

Urafiki wa kina wa Ujerumani na Marekani

Mkutano wa viongozi hao wawili pia unafuatia kile kilichobainishwa na mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, Jake Sullivan kwamba Marekani imekubali tu kupeleka Ukraine vifaru chapa Abrams, kwa sababu Ujerumani imeweka masharti ya kupeleka vifaru vyake chapa Leopard 2.

Scholz na Biden pia walitarajiwa kuzungumzia mzozo kuhusu ruzuku ya Marekani ya teknolojia za kijani zinazofaa kwa ajili ya hali ya hewa, chini ya Sheria ya Kupunguza Mfumuko wa Bei, IRA. Sheria hiyo ilisababisha gadhabu miongoni mwa washirika wa Marekani barani Ulaya, ambao wameelezea wasiwasi wao kwamba ruzuku hizo zinaweza kudhoofisha kampuni za Ulaya, wakati zikikabiliwa na athari kubwa kutokana na uvamizi wa Urusi.

Sudha David-Wilp, mkuu wa ofisi ya wakfu wa Marshall mjini Berlin anasema mkutano huo wa Ijumaa kati ya Scholz na Biden sio ishara ya mgogoro, bali ni fursa ya kuimarisha uhusiano binafsi kati ya viongozi hao wawili. ''Marekani bado inaitazama Ujerumani kama nchi inayoongoza kwa kuwa na nguvu kijeshi barani Ulaya. Ni fursa ya kujitathmini,'' alibainisha David-Wilp.

 

(DPA, AP, AFP, Reuters)