Safari ya kuelekea Brazil yaendelea barani Afrika | Michezo | DW | 14.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Safari ya kuelekea Brazil yaendelea barani Afrika

Mlinda lango wa Cameroon alifanya kazi ya ziada kuisaidia timu yake kutoka sare ya kutofungana bao na Tunisia katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa mechi za mchujo kufuzu katika dimba la dunia.

Tunisia walifanya shambulizi baada ya jingine, katika kipindi cha kwanza lakini kipa Itandje aliokoa makombora kadhaa. Nahodha wa Cameroon Samuel Eto'o, ambaye alirejea kikosini tena baada ya kusema kuwa anastaafu soka ya kimataifa, alikuwa mwiba katika safu ya ulinzi ya Tunisia.

Timu hizo mbili, ambazo zimefika katika kombe la dunia mara 10, zitamenyana tena katika mkondo wa pili mjini Yaounde mnamo Novemba 17, huku The Indomitable Lions wakipigiwa upatu kujikatia tikiti.

Kwingineko, Emmanel Emenike, alifunga mabao yote wakati Nigeria ilipowachabanga Ethiopia mabao mawili kwa moja na kuusongeza mguu mmoja katika tamasha la kombe la dunia kwa mara ya tano. Nao Burkinfa Faso waliyaweka hai matumaini yao ya kushiriki dimba la dunia kupitia ushindi wenye utata wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Algeria mjini Ougadougou siku ya Jumamosi.

Bao la ushindi katika dakika ya mwisho lilitokana na mkwaju wa penalti wake mchezaji Aristide Bance ambao kanda za video zinaonyesha kuwa penalti hiyo haikuwa halali. Mchezaji Essaid Belkalem alikuwa ameweka mikono yake nyuma mgongoni wakati mpira ulipogonga kifuani, lakini mwamuzi wamechi Mzambia akaamua kuwa ni penalti.

Nao vijana wa zamani wa Chelsea Didier Drogba na Salamon Kalou walikuwa miongoni mwa wafungaji wa ushindi wao wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Senegal. Gervinho, pia alichangia katika mabao yote matatu ya Cote d'Ivoire. Hapo kesho Jumanne, Ghana itaialika Misri katika mchuano unaosuburiwa kwa hamu kubwa wa mkondo wa kwanza.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters

Mhariri: Yusuf Saumu