Rwanda yawa mwanachama wa muda wa Baraza la Usalama la UN | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 19.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Rwanda yawa mwanachama wa muda wa Baraza la Usalama la UN

Rwanda imechaguliwa kuwa kiti cha mwanachama wa muda wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, licha ya nchi hiyo kushutumiwa na jopo la Umoja wa huo kuwaunga mkono waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Rais Paul Kagame wa Rwanda (Shoto) akiwa na Rais Joseph Kabila wa Kongo

Rais Paul Kagame wa Rwanda (Shoto) akiwa na Rais Joseph Kabila wa Kongo

Rwanda haikupingwa katika jitihada zake za kuwania kiti hicho kutoka Afrika kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo Afrika Kusini itamaliza muda wake mwezi Disemba mwaka huu, lakini bado ilikuwa inahitaji idhini ya theluthi-mbili ya kura za wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kupata kipindi cha muda wa miaka miwili. Rwanda ilishinda baada ya kupata kura 148 kati ya 193. Katika uchaguzi huo Argentina pia ilichaguliwa bila kupingwa baada ya kupata kura 182, huku Australia ikishinda kwa kupata kura 140. Luxembourg ilipata kura 131 na Korea Kusini kura 149.

Rwanda yazungumza baada ya kuchaguliwa

Baada ya kuchaguliwa katika chombo hicho cha Umoja wa Mataifa, Rwanda imesema itafanya kazi kwa kushirikiana na wanachama wote wa baraza hilo kuhakikisha inakuwa sikivu na kutafakari maoni na matarajio ya mataifa yanayoendelea. Kabla ya uchaguzi huo, ujumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo uliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa unapinga Rwanda kujiunga na Baraza la Usalama la umoja huo, huku ikiituhumu nchi hiyo jirani kwa kuwasaidia waasi wanaoendesha shughuli zao mashariki mwa Kongo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo

Ripoti ya siri ya jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa hivi karibuni imeeleza kuwa Rwanda na Uganda zinaendelea kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao wanapigana dhidi ya majeshi ya serikali ya Kongo kwa muda wa miezi sita sasa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rwanda imekuwa ikiwapatia silaha waasi hao pamoja na msaada wa kisiasa. Hata hivyo, Rwanda na Uganda zimekanusha vikali shutuma hizo.

Kabila apongeza ushindi huo

Kwa upande mwingine katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Paul Kagame wa Rwanda ametoa tamko la kuyapokea matokeo ya ushindi huo, akisema achilia mbali yanayosemwa na maadui, haki na ukweli vitajulikana na wakati mwingine vinahitaji mapambano kidogo kwa ajili ya hilo. Katika mahojiano yake na Shirika la Habari la Reuters, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo amezionya nchi dhidi ya kusitisha misaada kwa Rwanda kutokana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Akizungumza muda mchache baada ya Rwanda kushinda kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Bibi Mushikiwabo amesema litakuwa ni kosa kubwa sana kwa wafadhili kusitisha misaada kwa Rwanda. Aidha, amesema sasa Rwanda itakuwa tayari kuhakikisha amani inapatikana katika eneo la Mashariki mwa Kongo.

Nchi zilizositisha misaada

Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-Moon

Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-Moon

Marekani, Ujerumani, Sweden na Uholanzi zimesitisha misaada yao kwa Rwanda, nchi ambayo inategemea wafadhili kwa asilimia 40 ya bajeti yake. Mwezi uliopita Umoja wa Ulaya ulisitisha bajeti ya misaada kwa Rwanda. Hata hivyo, mwezi Septemba Uingereza ilifungua sehemu ya misaada yake kwa Rwanda, huku ikiipongeza nchi hiyo kwa kutafuta amani. Naibu Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Philip Parham amesema wako tayari kufanya kazi na Rwanda katika masuala ya amani ya kimataifa na usalama, ikiwemo juhudi za kuajribu kumaliza mzungumko wa ghasia Mashariki mwa Kongo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo /RTRE
Mhariri:Moahammed Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com