Rwanda yatupilia mbali wito wa kuondoa jeshi Kongo
19 Februari 2024Utawala nchini Rwanda umetupilia mbali hii leo wito wa Marekani wa kuondolewa kwa wanajeshi na mifumo ya makombora ya Rwanda huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ukisema wanalinda ardhi ya Rwanda hasa wakati huu Kongo ikijiimarisha kijeshi karibu na mpakani.
Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Rwanda imesema vitisho kwa raia na usalama wa taifa hilo, unatokana na kuwepo kwa waasi wa kundi la FDLR wenye silaha, ambao pia wamejumuishwa katika jeshi la Kongo na ambao wengi wao wanatuhumiwa kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Soma pia:Hali ya usalama yaendelea kuzorota Goma
Siku ya Jumamosi, Marekani ililaani hali ya kuongezeka kwa ghasia zinazofanywa na waasi wa M23 katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kusema wafuasi wa kundi hilo wanaoungwa mkono na Rwanda ni lazima waondoe makombora ya kisasa ya ardhini na angani ambayo yanatishia maisha ya mamilioni ya watu mashariki mwa nchi hiyo.