1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto aahidi nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi Kenya

1 Mei 2024

Wafanyakazi wanashusha pumzi baada ya serikali kutangaza nyongeza isiyopungua asilimia sita ya kima cha chini cha mshahara ili kuwapiga jeki.

https://p.dw.com/p/4fP2N
Rais wa Kenya William Ruto
Rais wa Kenya William RutoPicha: Simon Maina/AFP

Rais William Ruto alipanda jukwaani na kutangaza nyongeza isiyopungua asilimia ya kima cha chini cha mshahara. Kwenye hotuba yake, rais William Ruto alibainisha kuwa nyongeza hiyo inanuwia kuwapiga jeki wafanyakazi na kumtaka waziri wa Leba Florence Bore kufanikisha agizo hilo.

Itakumbukwa kuwa kwenye kongamano la tatu la taifa la masuala ya mshahara, Rais William Ruto alisisitiza kuwa azma ya serikali ni kupunguza gharama ya mishahara kutokea 51% hadi 35% katika muda wa miaka 3 ijayo. Kwa sasa mishahara imetengewa 46% ya pato zima la serikali.

Kadhalika ameitaka wizara husika kufufua mabaraza ya kujadili mishahara yanayoendana na sheria ya ajira ya 2007 ili kudumisha amani kazini na kusuluhisha migogoro ya wafanyakazi. Kauli hizo zinatolewa wakati ambapo mgomo wa madaktari na matabibu ulioanza katikati ya Machi mwaka huu ukiendelea.

Mgomo wa madaktari

Mgomo wa madaktari waendelea kwa wiki kadhaa
Mgomo wa madaktari waendelea kwa wiki kadhaaPicha: DANIEL IRUNGU/EPA

Madaktari wanadai nyongeza ya mshahara na mazingira ya kazi kuimarishwa. Kwenye hotuba yake ya Mwaka 2023 ya siku ya wafanyakazi, Rais William Ruto aliahidi mambo ya msingi yaliyolenga kuimarisha maisha ya wakenya. Kwanza kabisa alibainisha kuwa serikali yake itainyanyua sekta ya kilimo Kwa manufaa ya wakulima na kuunda ajira.

Moja ya mbinu za kufanikisha hilo ni kusambaza mbolea ya bei nafuu. Mpango huo sasa unaandamwa na kashfa ya mbolea bandia na waziri wa kilimo wa Kenya Mithika Linturi anasakamwa. Kwa sasa bunge la Taifalimeanzisha mchakato wa kutaka kumtimua. 

Siku ya wafanyakazi inaadhimishwa wakati serikali imeendelea kufyeka hela zaidi kupitia nyongeza ya kodi. Rais William Ruto alisisitiza kuwa serikali iko makini kuimarisha ukusanyaji ushuru ili kufanikisha miradi ya maendeleo na kupungua deni la taifa.

Hali ya mafuriko imedhibitiwa ?

Jiji la Nairobi laathirika na mafuriko baada ya mvua kubwa
Jiji la Nairobi laathirika na mafuriko baada ya mvua kubwa Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Wakati huohuo, mafuriko yanazitatiza kaunti kadhaa kufuatia Mvua inayoendelea kunyesha. Kaunti ya Nairobi ni moja ya zile zilizoathirika na gavana Johnson Sakaja anashikilia kuwa hali imedhibitiwa.

Kwa upande mwengine, muungano wa vyama vya wafanyakazi COTUunaandamwa na hoja ya kuweka vigezo vya muda wa viongozi kuhudumu.

Katibu mkuu wake Francis Atwoli alianza kuhudumu tangu 2001 na muda wake unakamilika 2026. Tayari mswada umeandaliwa kwenye baraza la Senate kujadili hoja ya kuweka muda maalum wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuhudumu.