Ronaldo aendelea kupepea katika La Liga | Michezo | DW | 11.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ronaldo aendelea kupepea katika La Liga

Cristiano Ronaldo alipachika bao katika mchezo wa kumi wa ligi ya Hispania msimu huu bila kukosa wakati viongozi wa ligi hiyo Real Madrid wakiirarua Rayo Valecano kwa mabao 5-1

Madrid sasa wamefikisha pointi 27 na magoli 42 katika michezo 11 ya La Liga. Barcelona imesogea hadi nafasi ya pili kwa ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Almeria, na kuiondoa Valencia katika nafasi hiyo baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Athletic Bilbao.

Chelsea imeendelea kutamba katika ligi ya Uingereza Premier League, ikifungua mwanya wa pointi nne na bila kufungwa msimu huu, baada ya kuwa nyuma kwa goli moja na kufanikiwa kushinda mchezo wake dhidi ya Liverpool kwa mabao 2-1.

Goli la Alexis Sanchez halikutosha kuweza kuipatia ushindi Arsenal London , baada ya kubadilishiwa kibao na Swansea na kuchapwa mabao 2-1 jana Jumapili na kuibua tena mjadala juu ya uwezo wa kocha wa siku nyingi wa klabu hiyo kongwe Arsena Wenger, ang'oke ama aendelee.

Hata hivyo kocha huyo wa Arsenal London amekiri kuwa hakuna cha kuizuwia Chelsea mara hii kunyakua ubingwa wa Premier League , baada ya kuiona timu yake ikikubali kipigo dhidi ya Swansea jana Jumapili. Zaidi ya theluthi mbili ya ligi bado haijachezwa na kuna uwezekanao wa pointi 81 kuwaniwa , lakini Wenger anaamini mahasimu hao wa mjini London hawazuiliki tena.

Kwingineko katika bara la Ulaya Juventus Turin imeendelea kushika usukani wa ligi ya Italia Serie A baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Parma ambayo iko mkiani mwa ligi, ikiwa ni ushindi wao wa 24 nyumbani mfululizo katika ligi hiyo.

Paris St. German ya Ufaransa imedhihirisha ubabe wake kwa Olympique Marseille jana baada ya kuibana na kuipa kipigo cha mabao 2-0.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afp / dpae / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com