1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mauaji ya watu 87 Sudan yazusha maandamano mapya

Sylvia Mwehozi
28 Julai 2019

Kamati iliyoundwa kufanya uchunguzi wa mauaji Sudan, imesema jumla ya watu 87 waliuawa na wengine 168 walijeruhiwa wakati vikosi vya usalama viliposhambulia maandamano ya amani katika mji mkuu wa Khartoum mnamo Juni 3.

https://p.dw.com/p/3MqTV
Sudan Khartum Proteste nach Razzi in Protestcamp
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Ukandamizaji huo ulitokea wakati maafisa wa ngazi ya juu walipokiuka amri iliyotolewa na Baraza la mpito la kijeshi TMC, amesema mkuu wa kamati hiyo ya uchunguzi iliyoundwa na TMC, Fath al-Rahman Saeed.

Kwenye ripoti yake mkuu wa tume hiyo Fath al-Rahman, amesema majenerali wanaongoza nchi hawakutoa amri ya kutawanya maandamano ya Juni 3 na kuwatuhumu askari wa kikosi cha kupambana na fujo RSF kwa ajili ya mauaji hayo. Ameongeza kuwa maafisa wanane kutoka kikosi hicho cha RSF walikaidi amri ya kutawanya maandamano ya amani mnamo Juni 3 katika mji mkuu wa Khartoum. Ingawa hakutoa maelezo ya kina ni jinsi gani uchunguzi utaendelea dhidi ya maafisa hao wanaotuhumiwa.

Aidha Fath al-Rahman, anasema vikosi vya usalama vilipewa maagizo ya kutawanya watu eneo la karibu na walikopiga kambi waandamanaji linaloitwa Colombia lakini sio kuvamia na kushambulia kambi hiyo kwa sababu ilikuwa ni alama ya vuguvugu lililochangia jeshi kumuondoa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir. Baraza la majenerali linaloingoza nchi limekuwa likisisitiza kwamba halikutoa amri ya kutawanya umati wa waandamanaji lakini lilitoa agizo ya operesheni ikiwemo ya RSF na vikosi vingine ya kusafisha eneo la Colombia ambalo wanasema lina shughuli za madawa ya kulevya na ghasia.

Demonstrationen im Sudan
Waandamanaji wakiwa mitaani siku 40 baaada ya mauaji ya Juni 3Picha: Reuters/M. N. Abdallah

"Waliondoa vizuizi, wakafyatua gesi ya kutoa machozi na kufyatua risasi kiholela na kusababisha mauaji ya waandamanaji na wengine kujeruhiwa na kuchomwa kwa matenti", alisema Fath al-Rahman.

Upinzani wakataa uchunguzi

Muungano wa upinzani wa uhuru na mabadiliko (FFC), hata hivyo umeikata ripoti ya kamati ukisema watu zaidi ya 100 waliuawa na kutaka uchunguzi huru. Mnamo Juni 3 askari waliokuwa wamevalia sare za kijeshi walivamia eneo ambalo waandamanaji waliketi hapo kwa muda mrefu, nje ya makao makuu ya jeshi na kuanza kuwafyatulia risasi na kuwapiga waandamanaji.

Nalo shirikisho la wanataaluma wa Sudan SPA,  limekataa uchunguzi huo likisema "uliagizwa na baraza la kijeshi lenyewe, na hii inatoa doa uadilifu wake kwasababu jeshi linatuhumiwa katika kesi hiyo". Nao waandamanaji waliojawa na ghadhabu waliandamana siku ya Jumamosi wakiikataa idadi iliyotolewa kama anavyosema mwandamanaji mmoja Amam al-Tahir, "uchunguzi huu hauna maana kwasababu tunafahamu kilichotokea dhidi ya waandamanaji".

Sudan Khartoum | Friedensgespräche
Baadhi ya viongozi wa baraza la kijeshi nchini SudanPicha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Awali, waandamanaji na makundi ya haki za binadamu yalikituhumu kikosi cha kupambana na ghasia cha RSF kwa ukandamizaji uliofanywa, lakini madai hayo yalikanwa na mkuu wa kikosi hicho Jenerali Mohamed hamdan Daglo. Lakini uchunguzi wa pamoja uliofanywa na waendesha mashitaka na baraza la kijeshi umedhihirisha kuwa kikosi hicho sambamba na vikosi vinginevyo vilishiriki mauaji ya Juni 3.

Umati wa waandamanaji ulopiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi kuanzia Aprili 6, wakilitaka jeshi kuungana nao kumuondoa Al-Bashir. Bashir aliondolewa Aprili 11, lakini waandamanaji waliendelea kupiga kambi wakilishinikiza baraza la kijeshi lililochukua madaraka kukabidhi kwa raia.

Mauaji hayo ya Juni 3 yalisababisha kuvunjika kwa mazungumzo baina ya jeshi na viongozi wa kiraia, lakini wiki kadhaa baadae mazungumzo hayo yaliendelea chini ya upatanishi wa Umoja wa Afrika na wanadiplomasia wa Ethiopia. Pande zote mbili zimekubaliana kugawana madaraka kwa kipindi cha mpito cha miezi 39.

Vanyo: AFP/AP/DPA