1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha usalama Sudan chahusishwa na ukatili Darfur

Saumu Mwasimba
11 Juni 2019

Shirika la Amnesty International limesema wanajeshi wa kikosi cha RSF kinachofungamana na wanamgambo wa Janjaweed wamehusika katika ukatili mkubwa wa kuua,kubaka na kuharibu vijiji Darfur

https://p.dw.com/p/3KBZH
Sudanesische Spezial-Polizei erwidert Beschuss von Rebellen
Picha: picture-alliance /dpa

Wakati Sudan ikiendelea kukabiliwa na mkwamo wa kisiasa,shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limetowa ripoti inayovinyooshea kidole vikosi vya usalama vya nchi hiyo kuhusika na uhalifu wa kivita na ukiukaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu katika jimbo la Darfur.

Ripoti ya Amnesty International inasema ukiukaji mkubwa na wakutisha wa haki za binadamu umefanyika Darfur na wahusika ni vikosi vya usalama vinavyojulikana kama RSF Rapid Support Forces. Hivi ni vikosi vinavyojumuisha wanamgambo waliotokana na kundi linalojulikana kwa ukatili mkubwa la Janjaweed lililoundwa katika miaka ya mwanzoni mwa 2000 wakati wa mgogoro wa Darfur na Omar al Bashir.

Shirika la Amnesty linasema ripoti yake imeandikwa kutokana na ushahidi mpya wa kutisha uliokusanywa ikiwemo picha za Satelaiti. Ushahidi huo ni pamoja na kuharibiwa kwa vijiji vyote pamoja na mauaji ya kinyama na ubakaji.

Sudan President Omar Hassan al-Bashir
Picha: Reuters/Z. Bensemra

Wanamgambo wa Janjaweed ni hatari wakikumbukwa kwa ukatili walioufanya na kwa kiasi kikubwa kutuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na Al Bashir ambaye sasa yuko Jela alihusishwa na kushtakiwa kwa tuhuma za mauaji ya halaiki. Lakini kamanda wa kikosi cha RSF jenerali Mohammed Hamdan Dagalo anayefahamika zaidi kwa jina la Hemedti sasa ndiye naibu mkuu wa baraza la kijeshi linaloshikilia madaraka nchini Sudan.

Viongozi wa mapinduzi wako katika mvutano mkubwa unaozidi kuzusha vurugu nchini humo na vuguvugu la waandamanaji  ambalo linataka baraza hilo la kijeshi liachie madaraka na kuukabidhi kwa serikali ya kiraia. Waandamanaji hawaonekani kuwa tayari kusalimu amri ,maduka na shughuli chungunzima zimeendelea kusimama kwa siku ya pili leo mjini Khartoum huku wakaazi wa mji huo wakishindwa kutoka nje. Hata hali katika mahospitali inatajwa kwamba imezidi kuwa mbaya.

UN Mission UNAMID
Picha: picture-alliance/dpa/S. Price

Wakati mvutano huu ukizidi kuchukua sura mpya Katibu mkuu wa Amnesty International Kumi Naidoo ametowa mwito kwa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutowapa kisogo watu wa jimbo la Darfur wanaowategemea walinda usalama wa Umoja wa Mataifa kwa usalama wao.Tamko hili limekuja hasa baada ya kusikika siku ya Jumatatu kwamba Umoja wa Mataifa umesema watawala wa kijeshi nchini Sudan wametoa amri ya kuutaka ujumbe wa UNAMID katika jimbo hilo la Darfur  ukabidhi ofisi zao kama sehemu ya hatua ya mpango wa kuondoka katika eneo hilo mwakani.