1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti: Vimelea vya Malaria vimekuwa sugu

Angela Mdungu
15 Aprili 2021

Watafiti leo Alhamisi wametoa ripoti kuhusu ushahidi wa kwanza wa kidaktari kwamba mabadiliko ya vimelea vyenye usugu dhidi ya dawa ndiyo chanzo cha ugonjwa wa Malaria kuendelea kuenea barani Afrika. 

https://p.dw.com/p/3s3qE
Ägyptische Mücke
Picha: picture-alliance/AP Photo/Oxitec, Derric Nimmo

Wataalamu wa dawa wamekuwa na wasiwasi kwa muda mrefu kuhusu kuibuka kwa tatozo la usugu dhidi ya dawa za kutibu Malaria barani Afrika, hali ambayo ilisababisha asilimia 90 ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo duniani kote kwa mwaka 2019

Utafiti uliochapishwa na jarida la kitabibu la Lancet unathibitisha wasiwasi huo. Katika majaribio ya kimatibabu, utafiti ulionesha kuwa Malaria ilionekana kudumu zaidi kwa watoto waliokuwa wakipokea matibabu ya kawaida  kama walikuwa wameathiriwa na vimelea vipya vya Malaria.

Ufanisi wa mchanganyiko wa dawa za Artemisinin ulikuwa mkubwa, lakini watafiti wanasema kuna haja kubwa ya ufuatiliaji zaidi nchini Rwanda ulikofanyika utafiti pamoja na mataifa jirani.

Dawa hii hufanya kazi kuondoa vimelea vya Malaria katika mwili wa mgonjwa ndani ya siku tatu na hutumiwa pamoja na dawa nyingine mshirika inayoondoa kabisa vimelea vilivyosalia.

Visa vya usugu vinaanza kuwa jambo la kawaida

Uganda AIDS
Picha: PETER BUSOMOKE/AFP/Getty Images

Mwandishi mkuu wa Utafiti katika kituo cha dawa cha kigali  Rwanda Biomedical center Aline Uwimana, anasema wamegundua kuwa visa vya usugu dhidi ya dawa vimeanza kuwa vya kawaida.

Usugu dhidi ya dawa ya artemisinin hutiliwa shaka kama vimelea vya Plasmodium falciparum vinavyosababisha Malaria vitaendelea kuwepo mwilini baada ya siku tatu za kuitumia.

Mwaka 2006 Rwanda ilianza kutumia dawa hiyo inayofahamika zaidi dhidi ya Malaria kama tiba ya awali dhidi ya Malaria.

Tafiti za mwaka 2013 na 2014 zilionesha mabadiliko kadhaa ya vimelea lakini hakuna ushahidi ulioonesha kuwa mchanganyiko wa dawa za artemisinin haukuwa na ufanisi.

Hata baada ya matibabu vimelea bado vinabakia mwilini 

Afrika Kinder Tabletten Medizin Gesundheit
Picha: Getty Images/Marco Di Lauro

Utafiti uliofuatilia hali hiyo wa mwaka 2018 hata hivyo, ulionesha kwa mara ya kwanza mabadiliko ya vimelea na kile kilichoitwa kuchelewa kuondoka kwa vimelea vya Malaria ingawa bado ufanisi wa dawa za Artemisinin ulibaki kuwa juu ya asilimia 90.

Katika majaribio, zaidi ya watoto 200 wa umri wa miezi sita hadi miaka mitano walioathiriwa na Malaria walipata matibabu ya siku tatu yaliyozoeleka na walikuwa chini ya uangalizi wa siku 28. Asilimia 15 kati ya hao waliendelea kuugua Malaria.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO, kuna takribani visa milioni 229 vya Malaria duniani kote. Ugonjwa huo uliwaua zaidi ya watu 400,000 mwaka 2019 huku theluthi mbili ya hao wakiwa ni watoto.