1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vitokanavyo na Malaria huenda vikaongezeka Afrika

Sylvia Mwehozi
23 Aprili 2020

Idadi ya vifo vilivyosababishwa na Malaria katika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara inaweza kuongezeka mara 2 hadi kufikia 769,000 mwaka huu, iwapo nguvu zote zitaelekezwa katika mapambano ya COVID-19.

https://p.dw.com/p/3bKQ6
Mücke, Blut saugend
Picha: picture-alliance/dpa/P. Pleul

Shirika la afya ulimwenguni WHO limeonya katika taarifa yake kwamba hadi sasa Afrika imethibitisha kesi zaidi ya 25,000 za virusi vya corona huku vifo vikipindukia 1200, na serikali kwa kushirikiana na WHO, zimejielekeza zaidi kwenye kupambana na janga la corona.

Mkurugenzi Mkaazi kanda ya Afrika Dr. Matshidiso Moeti amezitolea wito nchi zote za kiafrika kuhakikisha kwamba juhudi za kupambana na Malaria zinaendelea.

"Uchambuzi wa hivi karibuni ulibaini kwamba vyandarua vilivyowekwa dawa vimeachwa kusambazwa na udhibiti wa kesi umepungua, vifo vya malaria katika nchi za Afrika kusini mwa Sahara vinaweza kuongezeka mara mbili ukilinganisha na mwaka 2018”, alisema Moeti.

"Hii itakuwa idadi kubwa ya vifo kuwahi kushuhudiwa katika ukanda huo tangu mwaka 2000”, aliongeza mkurugenzi huyo. Pia aligusia juu ya takwimu za mripuko wa kirusi cha Ebola barani Afrika, na kuonyesha kwamba watu walikufa kutokana na maradhi mengine, ikiwemo malaria, kuliko hata Ebola yenyewe, kutokana na ukosefu wa upatikanaji matibabu.

Vifo vitaongezeka iwapo kasi ya kupambana na Malaria itapungua 

Medizin Forschung l Weltweit erste Malaria-Impfkampagne l Moskitonetz
Picha: picture alliance/dpa/E. Morrison

Mwaka 2018, kulikuwa na visa milioni 213 vya malaria na vifo 360,000 vinavyohusiana na ugonjwa huo katika kanda ya Afrika, ikiwa ni asilimia 90 ya kesi zote duniani. WHO imesema kama lengo la kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya corona itachangia kupungua kwa upatikanaji wa dawa za kupambana na malaria, vifo vitaongezeka mara mbili.

"Nchi katika ukanda mzima zina nafasi ndogo na fursa ya kupunguza uingiliaji katika udhibiti wa malaria, matibabu na kuokoa Maisha katika kipindi hiki cha mripuko wa COVID-19”, ilisema taarifa ya WHO.

Benin, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Sierra Leone na Chad zote zilianzisha programu za kupambana na malaria kipindi hiki cha mripuko wa corona, limesema WHO, na kuongeza kuwa nchi hizo zinapaswa kuwa mfano kwa mataifa mengine ya Afrika.

Chanzo: afp,reuters