Real Madrid wateleleka tena, Barcelona waongeza uongozi | Michezo | DW | 07.01.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Real Madrid wateleleka tena, Barcelona waongeza uongozi

Masaibu ya Real Madrid baada ya kuondoka kwa Zinedine Zidane kama kocha na mchezaji wao nyota Cristiano Ronaldo yaliendelea Jumapili, kwani walicharazwa magoli mawili bila jawabu na Real Sociedad.

Mechi hiyo ilichezwa uwanjani kwao Estadio Santiago Bernabeu katika ligi kuu ya Uhispania. Kutia msumari moto kwenye donda, Lucas Vazquez alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea mpinzani wake vibaya.

Kocha wa klabu hiyo Santiago Solari ambaye alionekana kama mkombozi baada ya kuondoka kwa Julen Lopetegui, alimlaumu sana muamuzi wa mechi hiyo kwa kushindwa kwao.

"Hapana, hatukuzungumza na muamuzi. Kuhusiana na mambo machache yaliyokuwa na mashaka, nafikiri baadhi yalionekana ya wazi kuliko mengine na nafikiri VAR imewekwa mahsusi kwa hali kama hizo - kama huna uhakika, uweze kupata ushauri."

Madrid waliingia kwenye mchuano huo wakiwa wametoka kulishinda taji la Kombe la Dunia la vilabu wiki mbili tu zilizopita na kila mmoja alitaraji kwamba watakuwa na kazi rahisi, licha ya kumkosa mchezaji wao nyote Gareth Bale aliyekuwa amejeruhiwa. Wachezaji wa Madrid walizomewa na mashabiki wao wenyewe katika muda wa mapumziko na hata mechi ilipokwisha lakini Solari hakuona sababu ya kuwalaumu vijana wake kwa mchezo usioridhisha.

Santiago Hernan Solari (picture alliance/AP Images)

Kocha wa Real Madrid Santiago Solari

"Ina maana gani teknolojia kama hii isipotumika? Bila shaka sote ni binadamu na sote tunaweza kufanya makosa, wachezaji, waandishi wa habari lakini ni jambo jengine iwapo unafanya kosa wakati una nafasi ya kulirekebisha. Kwa hiyo uspolirekebisha kosa hilo, nachanganyikiwa kidogo. Kwa hiyo ni vigumu kuelewa."

Kwengineko huko Uhispania mabao kutoka kwa Lionel Messi na Luis Suarez yalihakikisha kuwa vinara wa ligi kuu ya nchini humo Barcelona wanatoa ushindi wa magoli mawili kwa moja walipoingia uwanjani kucheza na Getafe ugenini.

Ushindi huo uliowahakikisha kwamba wanaongeza tofauti ya pointi kati yao na wanaowanyemelea Atletico Madrid waliokuwa wanacheza na Sevilla katika uwanja wa Ramon Sanchez Pizjuan. Mechi hiyo iliishia sare ya bao moja Wissam Ben Yedder akiifungua Sevilla goli lao kisha Madrid wakasawazishiwa na Antoine Griezzman. Barcelona sasa wana pointi arubaini wakiwa uongozini pointi tano mbele ya Atletico kisha Sevilla ni watatu na pointi 33 halafu Alaves wanaishikilia nafasi ya nne na Real Madrid ni watano.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE/DPAE

Mhariri: Gakuba Daniel