RB Leipzig bado yaonesha ubabe | Michezo | DW | 23.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

RB Leipzig bado yaonesha ubabe

Timu ya RB Leipzig iliyopanda daraja msimu huu imeendelea kuonesha kwamba hakuna wa kuiporomoa kutoka kilelele mwa ligi ikiisaka Bayern Munich iliyoko kileleni.

Fußball Bundesliga RB Leipzig v Eintracht Frankfurt (Reuters/F. Bensch)

Wachezaji wa RB Leipzig walipopambana na Eintracht Frankfurt

Katika  ligi  ya  Ujerumani Bundesliga , Bayer Leverkusen  imeanza vizuri mzunguko  huu  wa  pili  wa  Bundesliga  kwa  ushindi  mnono wa  mabao 3-1  dhidi  ya  Hertha BSC Berlin  jana  Jumapili . Bayer Leverkusen  ilishinda  jana  baada  ya  michezo  mitatu ya  nyumbani mfululizo  bila  ushindi  na  sasa  inamatumaini  ya  kupanda  na kushika  moja  kati  ya  nafasi  za  kuweza  kushiriki  michuano  ya Ulaya  msimu  ujao. Bayer  Leverkusen  imejikusanyia  hadi  sasa pointi  24  ikishika  nafasi  ya  nane  katika  msimamo  wa  ligi.  Kocha  wa  Leverkusen Roger Schmidt anasema,

Deutschland Bayer Leverkusen - Hertha BSC Hakan Calhanoglu (picture alliance/dpa/F. Gambarini)

Hakan Calhanoglu wa Leverkusen akishangiria bao pamoja na mchezaji mwenzake Omar Toprak

„Kwa  kweli  hatukucheza  vizuri  sana.  Lakini  hilo  halikutarajiwa.  Kuna mambo  machache  yaliyofanyakazi, ambayo yalitosha  kuweza  kushinda. Tulifanya  mambo  machache  vizuri , na  pia upo uwezo  wa   kufanya vizuri  zaidi.  Lakini  msingi  ulikuwapo. Nimeiona  timu  yangu , kuwa  ina uwezo mkubwa.  Ndio  sababu  nimefurahishwa."

Katika  mchezo mwingine  jana  wa  kukamilisha  duru  ya  michezo 17  ya mzunguko wa kwanza wa  Bundesliga  msimu  huu , FC Koln  ilipoteza  fursa  ya  kujipenyeza  katika nafasi  za  kucheza  katika  ligi  ya  Ulaya  msimu  ujao  baada  ya  kutoka sare  tasa  na  Mainz 05.

Deutschland FSV Mainz 05 - 1. FC Köln (picture alliance/dpa/T. Silz)

Mshambuliaji Anthony Modeste wa FC Kolon akipambana na Niko Bungert wa Mainz

Siku  ya  Jumamosi, RB Leipzig ilifanikiwa  kung'ang'ania  kileleni  mwa  ligi baada  ya  kuirarua Eintracht  Frankfurt  kwa  mabao  3-0 na  kujiweka pointi  tatu  tu  nyuma  ya  viongozi  wa  ligi  hiyo Bayern Munich, ambapo Bayern  sasa  ina  pointi  42  baada  ya  kuishinda Freiburg  siku  ya  Ijumaa kwa  mabao  2-1.  Borussia  Dortmund  ambayo imemsajili  leo kijana wa miaka  17  raia  wa  Sweden Alexander Izak  kwa  kitita  cha  euro  milioni 10  ilipata  ushindi  wa  kibarua  kigumu  dhidi  ya  Werder  Bremen  wa mabao 2-1.

Hoffenheim ni  timu  pekee  katika  ligi  kuu  za  bara  la  Ulaya  ambayo hado haijaonja  kipigo hadi sasa, na  siku  ya  Jumamosi  ilionesha  kuwa inaweza  kurefusha  rekodi  hiyo  kwa  kuikandika Augsburg  kwa  mabao 2-0. Hoffenheim  inaikaribisha  Leipzig  wiki  hii  katika  pambano  ambalo tayari  linasubiriwa  kwa  hamu.  Kocha  wa  Hoffenheim akizungumzia  ushindi   wa  timu  yake dhidi  ya  Augusburg, alisema.

"Kwa  msingi  wa  kipindi  cha  pili  tulistahili  kushinda. Tulicheza  kidogo kwa  tahadhari  zaidi. Kwa mtazamo  wangu  katika  kipindi  cha  kwanza tuliweka  tahadhari  mno, tulicheza  kwa  kumiliki  mpira  mno. Hali hiyo kwangu ilinikera kidogo."

 

Mwandishi:  Sekione  Kitojo / afpe / dpae /  rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahhman