Rajoelina ataapishwa jumamosi kuwa kaimu rais | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 19.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Rajoelina ataapishwa jumamosi kuwa kaimu rais

Kiongozi wa upinzani alietwaa mamlaka kisiwani Madagascar Rajoelina ameidhinishwa na mahakama kuu kuwa kaimu rais.

Kiongozi wa upinzani Andry Rajoelina alietwaa mamlaka kisiwani Madagascar.

Kiongozi wa upinzani Andry Rajoelina alietwaa mamlaka kisiwani Madagascar.

Mahakama kuu nchini Madagascar imemthibitisha Kiongozi wa upinzani, Andry Rajoelina, kuwa kaimu rais wa nchi hiyo. Sherehe za kumwapisha rasmi kaimu rais huyo zinatarajiwa kufanyika jumamosi ijayo.Uamuzi huo umepitishwa muda mfupi baada ya jeshi la kisiwa hicho kumkabidhi mamlaka kiongozi huyo wa upinzani.

Bwana Rajoelina anatarajiwa kuapishwa wakati ambapo pana wasiwasi mkubwa duniani juu ya uhalali wa hatua aliyochukua katika kutwaa mamlaka kutokana na kuungwa mkono na jeshi vilevile.Uhalali wa uongozi wake umesababisha utata zaidi kutokana na umri wake.Kwa mujibu wa katiba ya Madascar, umri wa miaka 34 wa bwana Rajoelina upo miaka sita chini ya umri wa kumfanya astahiki kuchaguliwa kuwa rais.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambae hapo awali alikuwa anawaburudisha watu kwa kuwapigia muziki- DJ, ametoa mwito wa kuleta umoja katika kisiwa cha Madagascar na ameazimia kupunguza bei ya chakula.

Bwana Rajoelina ametwaa mamlaka kutoka kwa rais wa hapo awali, Marc Ravalomanana.Mwanasiasa huyo kijana amesema ataiongoza nchi katika matayarisho ya kufanyika uchaguzi mnamo kipindi cha miaka 2 ijayo.

Bwana Rajoelina aliekuwa meya wa mji wa Antananarivo alitwaa mamlaka kwa uthabiti wote mapema wiki hii baada ya jeshi kupinga mpango wa rais Ravalomanana wa kukabidhi mamlaka hayo kwa jeshi.

Hatahivyo, jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi juu ya matukio ya kisiwani Madagascar.Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika inakutana leo nchini Swaziland kujadili matukio ya kisiwani humo.Watu wapatao 135 wamekufa kutokana na ghasia zilizotokea katika kisiwa hicho na kusababisha hasara ya dola milioni 390 katika sekta ya utalii.

Mwandishi: Abdu Mtullya-RTRE,AFP.ZA.

Mhariri: Miraji Othman.


 • Tarehe 19.03.2009
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HFNP
 • Tarehe 19.03.2009
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HFNP
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com