Rais Yanukovich kuzuru Ubelgiji | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais Yanukovich kuzuru Ubelgiji

Ataka kuihakikishia Ulaya kuhusu ajenda yake

Rais wa Ukraine Viktor Yanukovich

Rais wa Ukraine Viktor Yanukovich

Rais mpya wa Ukraine, Victor Yanukovich, katika ziara yake ya kwanza nje tangu alipoingia madarakani leo atazuru Ubelgiji katika jududi za kubadilisha mtazamo dhidi yake kama kibaraka wa Urusi na kujitokeza kama mtu anayeegemea Jumuiya ya Ulaya. Yanukovich aliyeapishwa kuwa rais alhamisi wiki iliyopita atakutana na rais wa umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy, mkuu wa kamisheni ya Ulaya Jose Manuel Barroso na mkuu wa sera za nje za umoja huo Catherine Ashton.

Wachunguzi wa mambo wanadai kwamba ziara ya kwanza nje ya rais Yanukovich nchini Ubelgiji badala ya Urusi atakakoelekea tarehe tano mwezi ujao, inaonekana kulenga kupunguza mtazamo wa kuegemea Urusi na kuihakikishia Ulaya kuhusu madhumuni yake.

Amanda Paul ambaye ni mchunguzi katika kituo cha masuala ya sera za ulaya mjini Brussels, amesema Yanukovich anahitaji kuonyesha kwamba yeye sio kibaraka wa Urusi.

Urusi ilikuwa inatarajia kuwepo uhusiano wa karibu na Ukraine chini ya utawala wa Yanukovich baada ya miaka kadhaa ya malumbano na rais wa zamani Victor Yushchenko aliyeegemea sana kambi ya nchi za magharibi.

Mchunguzi huru wa masuala ya kisiasa nchini Ukraine,Dmitry Vydrin amesema ziara ya Yanukovich inaweza kuchochea hisia za wivu mjini Moscow.

Katika maoni yanayoweza kufurahiwa mjini Brussels, swahibu wa rais huyo alisema kabla ya ziara yake kwamba Yanukovich hatarajii kuiweka Ukraine katika ushirikiano wa pamoja wa kibiashara unaungwa mkono na Urusi ukizijumuisha Belarus na Kazakhastan.

Irina Akimova ambaye ni naibu wa kwanza wa jeshi amesema muungano huo wa kibiashara utaathiri kwa kiasi kikubwa uanachama wa Ukraine katika shirika la biashara duniani, WTO. Katika maoni yaliyotumwa kwenye tovuti ya televisheni ya Inter nchini Ukraine, Akimova amesema suala hilo si jambo la leo, kesho wala kesho kutwa.

Urusi ilikuwa imependekeza awali kwamba Ukraine ingejiunga na muungano huo wa kibiashara lakini hatua kama hiyo italiudhi bara Ulaya ambalo lina mazungumzo na Ukraine kuunda kanda ya kibiashara na liko makini kuizuia Ukraine kutoegemea katika ushawishi wa Urusi.

Duru za ubalozi wa Ukraine, zilinukuliwa na shirika la habari la AFP ukisema kwamba, Ubelgiji imeshangazwa na uwezekano wa Ukraine kujiunga katika umoja wa forodha na Urussi kwa sababu itafufua muungano wa Kisovieti jambo ambalo lingebadilisha ramani ya Ulaya.

Ziara ya Yanukovich ilikuwa inatarajiwa sana na hakuna ziara yoyote iliyopangwa na iliyokuwa na matarajio makubwa kutoka upande wa Ulaya.

Ubelgiji itatarajiwa kuonyesha uungaji mkono wake kwa Ukraine, nchi ya zamani ya kisovieti yenye idadi ya raia milioni 46 ilioko kati ya Urusi na Ulaya, hasa baada ya miaka mingi ya ukosefu wa uhusiano wa karibu kati ya Ulaya na Ukraine.

Wakati huo huo Ubelgiji inatarajia Yanukovich atekeleze mageuzi ya kiuchumi yaliyokwamishwa na mzozo wa kisiasa nchini humo.

Mada nyingine itakayojadiliwa ni usambazaji wa gesi barani Ulaya kutoka Urusi inayopitia Ukraine. Umoja huo utahitaji kuhakikishiwa kwamba hakutatokea tena mzozo kati ya Urusi na Ukraine kama wa mwaka wa 2009 uliosababisha ukosefu wa gesi katika nchi kadhaa za Ulaya.

Nico Lange wa wakfu wa Konrad Adeneur mjini Kiev amesema kwamba Yanukovich pia anatarajiwa kujadili kuafikiwa kwa makubaliano kati ya kampuni ya nishati ya Urusi ya Gazprom na nchi za Ulaya kukarabati mabomba ya gesi nchini Ukraine jambo ambalo Urusi haingeweza kushiriki chini ya utawala wa Yushchenko.

Mwandishi, Peter Moss/ AFP

Mhariri, Saumu Mwasimba

 • Tarehe 01.03.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MEsL
 • Tarehe 01.03.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MEsL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com