Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff hana hatia | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff hana hatia

Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff Alhamisi(27.02.2014) amefutiwa mashtaka ya rushwa katika kesi ambayo ilisababisha kujiuzulu kwake miaka miwili iliopita na kumfadhaisha Kansela Angela Merkel aliyempendekeza.

Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff baada ya kufutiwa mashtaka ya rushwa katika mahakama ya Hannover.(27.02.2014).

Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff baada ya kufutiwa mashtaka ya rushwa katika mahakama ya Hannover.(27.02.2014).

"Mshtakiwa Wulff ameonekana kutokuwa na hatia " hivyo ndivyo jaji aliyeisimamia kesi hiyo Frank Rosenow alivyoiambia Mahakama ya mkoa ya Hannover na kuongeza kusema Wulff anastahiki kulipwa fidia kutokana na upekuzi uliofanywa na polisi nyumbani kwake.

Jaji huyo amesema kwa kweli hakuna ushahidi madhubuti dhidi ya washtakiwa.

Wulff mwenyewe amewaambia waandishi wa habari kufuatia hukumu hiyo kwamba amefarajika na kamwe alikuwa hana wasi wasi wote juu ya matokeo yatakavyokuwa.

Hukumu hiyo inakamilisha tamthiliya ya kisheria na kisiasa kwa nyota iliokuwa ikin'gara na kuanguka kutokana na madai ya kupokea vijitakrima kutoka kwa marafiki zake matajiri na kujaribu kuvinyamazisha vyombo vya habari kwa kutumia vitisho.

Kutunza heshima yake

Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff akiwasili katika mahakama ya Hannover.(27.02.2014).

Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff akiwasili katika mahakama ya Hannover.(27.02.2014).

Wulff mwenye umri wa miaka 54 ambaye alikuwa rais kijana kabisa kuwahi kushika wadhifa huo nchini Ujerumani alikuwa amesisitiza juu ya kutokuwa na hatia kwake na mwaka jana alikataa pendekezo la kuimaliza kesi hiyo kwa kulipa faini ya euro 20,000 na badala yake aliapa kulisafisha jina lake na kutunza heshima yake.

Mwanzoni mwa kesi yake hiyo hapo mwezi wa Novemba Wulff alielezea kusononeshwa kwake na madai dhidi yake na alidai kupatiwa haki kwa kusema kwamba idhara binafsi aliyoipata yeye na familia yake itaendelea kubakia pengine hata milele.

Kwa kulinganisha na kashfa za kisiasa ambazo zimegonga vichwa vya habari mahala pengine duniani madai yaliokuwa yakimkabili rais huyo wa zamani wa Ujerumani yaliwashangaa wengi kwa kule waendesha mashataka kujenga kesi yao kwa malipo ya takrima yasiozidi euro 700.

Gharama hizo zilitumika kwa ajili ya chumba cha hoteli, kuangalia watoto na chakula mkahawani ambapo mtenegezaji filamu David Groenworld mwenye umri wa miaka 40 ambaye pia ameshtakiwa anadaiwa kuilipa familia ya Wulff wakati wa ziara waliofanya kwa pamoja mjini Munich wakati wa Tamasha la mwezi wa Oktoba.

Maisha ya faragha

Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufutiwa mashtaka ya rushwa Hannover.(27.02.2014).

Rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufutiwa mashtaka ya rushwa Hannover.(27.02.2014).

Tokea ajiuzulu kutoka wadhifa huo wa urais ambao nchini Ujerumani ni wa heshima na sio wa utendaji hapo mwezi wa Februari mwaka 2012, Wulff amekuwa akiishi kwenye maisha ya kujitenga na alikuja kuvuta tena nadhari ya vyombo vya habari wakati alipokuja kutengana na mke wake mrembo ambaye alikuwa mama rais Betina Wulff.

Kashfa ya kisiasa ya Wulff ilianza kwa kubainika kuwa alishindwa kutangaza mkopo rahisi wa nyumba hapo mwaka 2008 aliopewa na mke wa rafiki yake tajiri na kufuatiwa na mfululizo wa repoti kuhusu vijifadhila vyengine alivyokuwa akikirimiwa ikiwa ni pamoja na mapumziko ya anasa.

Wulff alizidi kuichafuwa hali hiyo kwa kwanza kukanusha madai dhidi yake na kuonekana kujaribu kuwatisha waandishi wa habari kwa nia ya kuwanyamazisha ambapo aliacha ujumbe wa sauti kwa mhariri anayetambulikana wa gazeti mashuhuri kabisa nchini Ujerumani la Bild.

Baadhi ya wachambuzi wanaiona kesi hiyo ambayo imewahusisha mashahidi chungu nzima na maelfu ya kurasa za ushahidi imetowa ishara kwamba hakuna afisa wa serikali ya Ujerumani aliye juu ya sheria hata kama ni rais.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com