Rais wa Marekani kuhutubia Umoja wa Afrika mjini Addis Abeba | Matukio ya Afrika | DW | 28.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais wa Marekani kuhutubia Umoja wa Afrika mjini Addis Abeba

Rais Barack Obama wa Marekani atahutubia Umoja wa Afrika - kilele cha ziara yake fupi iliyomfikisha Kenya na baadae nchini Ethiopia - ziara iliyogubikwa na masuala kuhusu usalama na haki za binaadam.

Barack Obama in Äthiopien

Rais Barack Obama wa Marekani zirani nchini Ethiopia

Kabla ya kuhutubia Umoja wa Afrika,rais Barack Obama amepangiwa kutembelea kiwanda cha chakula nchini Ethiopia.Nchi hiyo ya Mashariki ya Afrika inapokea misaada mingi zaidi ya dharura na kuendeleza mazao ya chakula kutoka Marekani na ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki katika mradi wa Marekani wa kupambana na njaa kote ulimwenguni.

Ethiopia pia ndiko yanakokutikana makao makuu ya Umoja wa Afrika ambako rais Obama anapanga kuwahutubia viongozi wote wa bara hilo kutoka jengo jipya la makao makuu hayo mjini Addis Ababa.

Mshauri wa rais Obama wa masuala ya usalama Susan Rice amesema Umoja wa Afrika unashikilia nafasi ya juu katika masuala kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na amani na usalama,afya na kilimo.Ameongeza kusema kwamba rais Barack Obama anataka kuutembelea Umoja wa Afrika na kulihutubia bara la Afrika kwa sababu Marekani inataka kushirikiana kwa dhati zaidi na Umoja wa Afrika katika masuala kadhaa miongoni mwa hayo.

Rais Obama atarajiwa kufafanua fikra yake kuhusu maendeleo barani Afrika

Afrikanische Union 24. Gipfeltreffen in Addis Abeba

Viongozi wa Umoja wa Afrika wakikutana katika makao makuu ya Umoja huo mjini Addis Abeba

Muda mfupi kutoka sasa rais Barack Obama ataingia katika ukumbi wa Nelson Mandela na kuwahutubia viongozi wa Afrika.Ataitumia fursa hiyo kufafanua fikra yake kuhusu maendeleo barani Afrika,ufumbuzi wa mizozo inayoendelea barani humo na kukumbusha ahadi za Marekani,mwaka mmoja baada ya mkutano wa kilele kati ya Marekani na Afrika,mwezi Agosti mwaka 2014.

"Ni ziara ya kihistoria na hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya Umoja wa Afrika na Marekani-amesema mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika bibi Nkosazana Dlamini Zuma kabla ya rais Obama kuwasili katika makao makuu ya Umoja wa Afrika.Rais Obama amepanga pia kuonana ana kwa ana na bibi Dlaimini Zuma.

Mradi "Power Africa ulioanzishwa na Barack Obama kwa lengo la kuzidisha mara dufu uwezo wa watu kupata nishati ya umeme barani Afrika hadi ifikapo mwaka 2018,bado unazorota na rais Obama anapanga kuyahimiza makampuni ya Marekani yawekeze zaidi barani humo.

Mashirika ya kiraia yanataraji rais Obama atawahimiza viongozi wa Afrika waheshimu muongozo wa Umoja huo

Nkosazana Dlamini-Zuma

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika bibi Nkosazana Dlamini- Zuma

Katika wakati ambapo bara la Afrika linakabwa na mizozo ya kila aina kuanzia Burundi,kupitia Sudan Kusini na jamhuri ya Afrika kati,mashirika ya kiraia yanataraji rais Obama atauhimiza Umoja wa Afrika ushadidie umuhimu wa kuheshimiwa zaidi mwongozo wa Umoja huo kuhusu mfumo wa kidemokrasia,chaguzi huru na utawala bora.

Hotuba ya rais Barack Obama itakamilisha ziara ya siku tano katika mataifa mawili ya Afrika mashariki iliyoanza Kenya ijumaa iliyopita,nchi alikozaliwa marehemu babaake.Rais Obama ataondoka Ethiopia mara baada ya hotuba yake katika makao makuu ya umoja wa Afrika na anatarajiwa kuwasili Washington mapema kesho .

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba