1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Afghanistan azindua mpango wa amani na Wataliban

Sylvia Mwehozi
28 Februari 2018

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amezindua mpango wake wa mazungumzo ya amani na Wataliban, ambao unaweka uwezekano wa kulitambua kundi hilo kama chama cha kisiasa

https://p.dw.com/p/2tSC3
Afghanistan Kabul Friedens-Konferenz
Picha: Reuters/O. Sobhani

Hatua hiyo inajiri siku baada ya kundi hilo la waasi kuitisha mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani. Kwenye tamko lake la kuutangaza mpango huo wa maridhiano, ambalo limetolewa katika kongamano linalozishirikisha nchi 25, Rais Ghani amekaribisha ushirikishwaji wa Pakistan, ambayo imeshutumiwana Marekani na maafisa wa Afghanistan kwa muda mrefu kwa kuwapa waasi wa Taaliban ulinzi. Ghani amesema kuwa mataifa hayo mawili yanaweza kusahau tofauti zao za nyuma na kufungua ukurasa mpya wa mahusiano yao.

Wataliban hawakualikwa kongamano, Kabul

Hata hivyo waasi wa Taliban hawakukaribishwa kwenye kongamano hilo, lakini duru zimeliambia shirika la habari la dpa kuwa Jan Mottasim, aliyekuwa waziri mwenye mamlaka makuu katika serikali ya Taliban hadi mwaka 2001 alikuwa amealikwa. 

Afghanistan Taliban-Gruppe unterstüzt TAPI-Projekt- Mulla Ayoub
Mulla Ayoub, Kamanda wa kundi la Wataliban waliotengwaPicha: DW/S. Tanha

Inaripotiwa kuwa Mottasim amekuwa msuluhishi watofauti kati Afghanistan na wataliban siku za nyuma. Mapema msemaji katika wizara ya mambo ya nje wa Afghan alisema kuwa waakilishi katika mataifa  na mashirika matatu yakimataifa yanayohudhuria kongamano hilo yanajaribu kutafuta njia za kuleta kundi la waasi la Taliban kwenye meza ya mazungumzo.

Kongamano hilo linafanyika chini ya ulinzi mkali. Kwa mujibu wa takwimu za Marekani na Afghanistan, Wataliban wanadhibiti asilimia 13 ya Afghanistan huku duru nyingine zikisema kuwa waasi hao wanadhibiti asilimia 40 ya taifa hilo.

Mara kwa mara waasi Wataliban wamekataa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na serikaliya Afghanistan wakiita kuwa ni vibaraka na badala yake kutaka kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani ambayo imepeleka idadi kubwa ya vikosi vya kulinda Amani nchini humo. Kundi hilo lilirejelea wito huo wake siku ya Jumatatu. 

Raia waathirika

Idadi ya raia waliojeruhiwa imekuwa ikiongzeka katika miezi ya hivi karibuni, huku Wataliban wakiendelea kulenga miji, kama jibu kwa sera ya makabiliano ya Marekani iliyoagizwa na rais Donald Trump.

Afghanistan Anschlag auf Moschee in Herat
Raia wa Afghanistan wakumbwa na taharuki baada ya mlipuko kutokea Picha: DW/S. Tanha

Katika kongamano hilo linalofanyika mjini Kabul, Rais Ghani alisema kuwa iwapo mpango wake utakubaliwa na Wataliban, basi wanastahili kutambua serikali ya Afghanistan pamoja na katiba, masuala tata ambayo yamekuwa vizuizi kwa mazungumzo siku za nyuma.

Mtaalam wa masuala ya Taliban ambaye pia ni mwanahabari wa Pakistan Rahimullah Yusufzai amesema kuwa uongozi wa waasi unashikilia msimamo wake wa kufanya mazungumzo na Marekani pekee, lakini wengine kwenye kundi hilo wana Imani ya kufanya mazungumzo na Kabul.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Matifa, vita katika taifa hilo vimekuwa na athari kubwa, huku raia wake 460,000 wakilazimishwa kutoroka kwao tangu mwaka uliopita na raia wengine 10,000 wakiuawa ama kujeruhiwa. 

Serikali ya Afghanistan imekataa kuchapisha idadi ya wanajeshi wake waliouawa kwenye mzozo huo, mwaka 2017,  japo mwaka 2016, idadi hiyo ilikuwa Zaidi ya 8,000,huku waliojeruhiwa ikiwa 14,000.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Afp, Dpa

Mhariri: Daniel Gakuba