1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara yake inatokea katikati ya mauaji yanayofanywa na waasi

John Kanyunyu6 Oktoba 2020

Waasi kutoka Uganda ADF wamewauwa watu 11 jana katika kijiji cha Mamove, kilomita zaidi ya arubaini kaskazini magharibi ya mji wa Beni.

https://p.dw.com/p/3jUho
Demokratische Republik Kongo Kinshasa | Präsident | Félix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi Picha: G. Kusema

Mauaji hayo yanatokea wakati rais wa Congo Félix Tshisekedi yuko ziarani katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini.

Mauaji hayo ya watu 11, yamepelekea baadhi ya wakaazi wa kijiji cha Mamove kuyahama makaazi yao na kukimbilia mahala ambako wanadhani kwamba kuna usalama.

Akizungumza na idhaa ya DW Kiswahili kwa njia ya simu, mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika kijiji cha Mamove, katika wilaya ya Beni, Dinos Katuo anatupatia hali inayojiri katika kijiji hicho, huku akiwaomba viongozi wa jeshi kufanya juu chini, ili kuwalinda raia pamoja na mali zao. Amesema: "Hali ni mbovu kabisa. Viongozi wanajuwa wajibu wao, wanapaswa kulinda raia pamoja na mali yake. Tazama kwa sasa, Mamove imeachwa na wakaazi wake. Najiuliza je, askari watalinda hasa nyumba au miti. Wanapaswa kusuka mikakati ili kumtokomeza adui anayeharibu usalama wa wananchi."

Idadi ya watu waliouawa imeongezeka hadi 939

Symbolbild Opfer der ADF
Ibada ya mazishi ya watu waliouawa na waasi wa ADFPicha: Getty Images/AFP/K. Mailro

Ifahamike kwamba, mauaji ya watu hao 11, yamepelekea idadi ya waliouawa katika wilaya ya Beni kuongezeka na kufikia mia tisa na thelathini na tisa, tangu zilipoanza operesheni kabambe za kijeshi dhidi ya ADF, Oktoba 30 mwaka uliopita.

Na huko hayo yakiwa namna hiyo, rais Félix Tshisekedi yuko ziarani katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, kutathmini hali ya usalama katika eneo la mashariki ya Congo, kwa mujibu wa duru zilizo karibu na ikulu ya rais.

Ziara hiyo inayoanzia mji wa Goma inaaminiwa na wengi kwamba itampeleka katika maeneo ya Beni na Bunia Ituri, ambako mauaji ya wakaazi yanafanywa na makundi ya waasi na kubwa katika yote likiwa ni kundi la ADF waasi kutoka Uganda.

Na akizungumza na idhaa hii, akitaka libanwe jina lake, mmoja wa viongozi wa mashirika ya kiraia amesema, kuwa ni jambo la busara kwa rais Félix, kukadiria operesheni za kijeshi dhidi ya ADF kwani, matunda yaliyotarajiwa kutoka operesheni hizo kabambe yaani amani bado kupatikana, ijapokuwa serikali ilitoa pesa nyingi, ili kufanikisha nia ya rais ya kuona amani inarudi katika mji na wilaya ya Beni jambo lililodhaniwa kuwa litasimamisha mauaji ya wakaazi.

 

Mwandishi: John Kanyunyu