1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia: Vurugu za uchaguzi zililenga kuiangusha serikali

Imechapishwa 2 Desemba 2025ilisahihishwa mwisho 2 Desemba 2025

Katika hotuba yenye ujumbe mzito wa kiusalama, Rais Samia Suluhu Hassan amefichua kuwa vurugu za uchaguzi ziliratibiwa na watu wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuibomoa serikali, na kuzionya vikali taasisi za dini.

https://p.dw.com/p/54bLG
Tanzania Dar es Salaam 2025 | Rais Samia Suluhu Hassan akizumgumza na Wazee wa Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia Baraza la Wazee wa Dar es Salaam, Desemba 02, 2025, amesema machafuko ya Oktoba 29 yalipangawa na watu wa ndani na nje ya Tanzania.Picha: State House
Ruka sehemu inayofuata Unachohitaji kujua

Unachohitaji kujua

  • Rais Samia azionya taasisi za dini: Msijivishe mamlaka ya kuyasemea madhehebu mengine
  • Rais Samia: Vurugu ziliratibiwa na watu wa ndani na nje
  • Rais Samia: Sifa yetu ya kisiwa cha amani iko hatarini
  • Rais Samia Suluhu Hassan ahutubia taifa kupitia Baraza la Wazee wa Dar es Salaam
Ruka sehemu inayofuata Rais Samia: “Wakati wowote wakija, tumejipanga”
2 Desemba 2025

Rais Samia: “Wakati wowote wakija, tumejipanga”

Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali iko tayari kukabiliana na jaribio lolote la kuendeleza maandamano au machafuko nchini, akifichua kuwa mmoja wa waandaaji wa vurugu hizo ameshauri kundi lake kuepuka tarehe 9 Desemba na badala yake kupanga maandamano tarehe 25 Desemba. “Nataka niwaambie, wakati wowote wakija—tumejipanga,” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa baadhi ya wahusika wamekuwa wakituma salamu serikalini wakitoa masharti ya kuzungumza, lakini akasisitiza kuwa serikali haitalazimishwa wala kupewa masharti na mtu yeyote. “Serikali hii haiwezi kuamrishwa. Sisi ni nchi huru,” amesema.

Rais Samia amesema pia kuwa wapo wanaoishinikiza serikali “imuachie mtu fulani” kama sharti la maridhiano, jambo alilokataa akisema maridhiano hayataongozwa kwa mashinikizo kutoka nje. Ameongeza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishinda uchaguzi kwa asilimia 97, na kwamba wanaouliza kwa nini asilimia hiyo ni kubwa “hawakuwepo kwenye uchaguzi,” hivyo hawapaswi kutilia shaka maamuzi ya waliojitokeza kupiga kura.

Amesisitiza kuwa pamoja na jeraha lililotokana na vurugu zilizopita, Watanzania wenyewe ndiyo watakaolitibu—kupitia majukwaa ya mazungumzo, ushirikiano wa wazee, na kuwaongoza vijana kutojiingiza kwenye mipango ya kuchochewa.

Ametoa wito: “Tukae tuzungumze. Wazee wetu na vijana wetu wasitumike. Tanzania itajengwa na Watanzania.”

https://p.dw.com/p/54c09
Ruka sehemu inayofuata Rais Samia azionya taasisi za dini: “Msijivishe mamlaka ya kuyasemea madhehebu mengine”
2 Desemba 2025

Rais Samia azionya taasisi za dini: “Msijivishe mamlaka ya kuyasemea madhehebu mengine”

Rais Samia Suluhu Hassan amezionya taasisi za dini ambazo, kwa namna moja au nyingine, amesema zimejiingiza kwenye mkumbo wa mijadala na matamko yanayochochea mgawanyiko nchini. Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema Tanzania haina dini rasmi, lakini wananchi wake wana dini mbalimbali, na hakuna dhehebu lililopewa mamlaka ya kuyatamka au kuyazidi madhehebu mengine kisheria.

Amesema dini kuu nchini—akiwaelekeza viongozi wa madhehebu—hazijapewa uwezo wa kutoa matamko yanayojipenyeza kuonekana kama yanawakilisha madhehebu yote. “Viongozi wa dini msijivishe majoho ya kuonesha kuwa mnaweza ku-override madhehebu mengine,” alisema.

TEC yataka wahusika wa mauaji Tanzania kuwajibishwa

Akilitaja moja kwa moja Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Rais Samia alisema limekuwa likitoa matamko mara kwa mara, ikiwemo manane yaliyotolewa katika kipindi kifupi. Hata hivyo, amesema hata ndani ya TEC kuna viongozi wanaopinga matamko hayo wakiyaita batili, jambo analosema linaonesha kuwa msimamo huo si wa taasisi nzima.

Amesema mafundisho ya dini zote yanasisitiza kuwa mamlaka yoyote huwekwa na Mungu, iwe inashikiliwa na kiongozi mwanamke au mwanaume. Kwa msingi huo, amewataka viongozi wa dini “kuvaa majoho yao” na kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kiroho bila kuingia katika mivutano ya kisiasa inayoweza kuhatarisha amani.

Rais Samia amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa dini, lakini pia inatarajia taasisi hizo kuheshimu mipaka ya majukumu yao na kuchangia kujenga mshikamano wa taifa, si kuuteteresha.

https://p.dw.com/p/54bx2
Ruka sehemu inayofuata Rais Samia: “Vurugu ziliratibiwa na watu wa ndani na nje – wengine niliwanyoshea mkono wa rehema”
2 Desemba 2025

Rais Samia: “Vurugu ziliratibiwa na watu wa ndani na nje – wengine niliwanyoshea mkono wa rehema”

Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali haijawazuia wapinzani kushiriki uchaguzi, na kwamba waliokataa kushiriki walifanya hivyo kwa uamuzi wao wenyewe. Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais Samia alihoji sababu ya baadhi ya watu kuchochea vurugu “siku ya uchaguzi” badala ya kutumia njia halali za kisiasa.

Amesema serikali ina taarifa kuwa vurugu hizo ziliratibiwa na watu walioko nje ya nchi, na uchunguzi unaendelea kubaini majina zaidi. Kwa upande wa waratibu wa ndani, Rais Samia amesema baadhi yao ni watu wanaokabiliwa na changamoto za maisha, lakini wengine ni watu wasio na shida yoyote, “bali wanalipwa na wale wanaotaka machafuko yatokee.” Amesema baadhi ya wahusika “hata si Watanzania kikamilifu.”

Mahojiano maalum ya DW na rais Samia Suluhu Hassan

Rais Samia ameeleza kuwa mpango huo wa vurugu ulipangwa kwa uratibu wa hali ya juu, huku wahusika wakidai wana madai halali. Hata hivyo, amesema wengi wao ni watu wenye migogoro ya muda mrefu kwenye vyama vyao, waliohama au kugawanyika, na sasa wanaitupia serikali lawama zisizo za haki.

 “Hawa hawa mwaka 2020 niliwanyoshea mkono wa rehema. Niliwakuta nje wanateseka, nikawapa hata posho yangu ya safari. Niliwaahidi kuwafutia kesi na kuwapa kianzio. Niliwafungulia kila kitu. Leo, ambaye aliwafungulia ndiye wanayemgeuza kuwa mbaya,” alisema Rais Samia.

Amesema pamoja na hayo yote, serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda amani na kuhakikisha siasa za ushindani zinakwenda kwa mujibu wa sheria bila kuruhusu mpango wowote wa uchochezi kuvuruga nchi.

https://p.dw.com/p/54bu1
Ruka sehemu inayofuata Rais Samia: “Vurugu Zilikuwa Mradi wa Kutaka Kuiangusha Serikali”
2 Desemba 2025

Rais Samia: “Vurugu Zilikuwa Mradi wa Kutaka Kuiangusha Serikali”

Rais Samia Suluhu Hassanamesema vurugu zilizotokea nchini hivi karibuni hazikuwa za kawaida, bali ni tukio lililopangwa kwa makusudi na watu wenye dhamira ya kuangusha serikali. Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema wahusika walitaka Tanzania kupitia machafuko kama yale yaliyowahi kutokea Madagascar.

Amesema vurugu hizo zilikuwa “mradi wa wasioitakia Tanzania mema,” na kwamba baadhi ya watu walilipwa fedha ili kuingia mitaani na kuanzisha maandamano yenye lengo la kusababisha taharuki na uharibifu mkubwa. Matokeo ya machafuko hayo, amesema, ni pamoja na kuchomwa kwa majengo kadhaa, vituo vya mafuta, vituo vya polisi na mali binafsi.

Rais Samia atoa wito wa mshikamano wa kitaifa

Rais Samia amehoji kama vitendo hivyo vinafanana kwa vyovyote na maandamano yanayoelezwa katika katiba, akisema: “Kuunguza vituo vya polisi na biashara za watu—hivi ndivyo tunaita maandamano ya kikatiba?”

Akizungumzia matumizi ya nguvu yaliyofanywa na vyombo vya dola, Rais Samia amesema serikali ina wajibu wa kulinda nchi na mipaka yake, na kiwango cha nguvu hutegemea ukubwa wa tukio linalotokea. “Wanaosema tulitumia nguvu kubwa, swali ni—nguvu ndogo ndiyo ipi?” ameuliza.

Amesema wale wanaoikosoa serikali walitaka vyombo vya usalama “vikae na kutazama mpaka umati ukamilishe kile walichotumwa.” Ameeleza kuwa serikali haitasita kutimiza wajibu wake wa kulinda amani na usalama wa nchi, na itaendelea kufanya hivyo bila kuyumba.

https://p.dw.com/p/54bc2
Ruka sehemu inayofuata Rais Samia aonya: “Sifa yetu ya kisiwa cha amani iko hatarini”
2 Desemba 2025

Rais Samia aonya: “Sifa yetu ya kisiwa cha amani iko hatarini”

Tanzania Dodoma | Ras Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan amesema vurugu ziliifanya Dar es Salaam isimamePicha: AFP

Rais Samia Suluhu Hassan amesema sifa ya Tanzania kama kisiwa cha amani iko hatarini kufifia kufuatia matukio ya vurugu yaliyoshuhudiwa hivi karibuni. Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema amani na ukarimu ndiyo utambulisho wa taifa, lakini “kila siku zinavyokwenda, sifa yetu inapooromoka.”

Ameonya kuwa kuna watu “wasioitakia mema nchi” ambao wanachochea migogoro na kuhatarisha usalama wa raia. Rais Samia amesema Watanzania hawana sababu ya kuumizana wala kunyimana uhuru, akisisitiza kuwa damu ya Mtanzania “ni dhamana ya wote” na haipaswi kumwagika bila sababu.

Ametoa wito kwa wananchi kuwa watulivu, wenye busara na kuilinda amani ya nchi kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

https://p.dw.com/p/54bbJ
Ruka sehemu inayofuata Wazee wa Dar es Salaam wampongeza Samia kwa ushindi, uongozi mahiri
2 Desemba 2025

Wazee wa Dar es Salaam wampongeza Samia kwa ushindi, uongozi mahiri

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Dar es Salaam, Mzee Salumu Matimbwa, amempongeza Rais Samia kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu, akisema ushindi huo unaonesha wazi kuwa yeye ni kiongozi mahiri.

“Sisi wazee wa Dar es Salaam tunatambua kwamba kampeni zilikwenda vizuri kwa vyama vyote vilivyoshiriki. Kampeni ziliendelea salama hadi pale kundi dogo lilipojitokeza na kuanza kufanya uharibifu,” alisema Mzee Matimbwa, akiongeza kuwa wao kama wazee wamefadhaishwa na tukio hilo.

Aidha, Mzee Matimbwa alimshukuru Rais kwa kuonesha uongozi bora kupitia namna alivyoshughulikia kadhia hiyo, ikiwemo kuunda tume ya uchunguzi ili kubaini kiini cha vurugu hizo na kuweka wazi ukweli. Pia alimpongeza kwa kuendelea kuwaasa vijana kuwa nguzo muhimu ya kulinda amani ya nchi.

Amesema wazee wamefurahishwa pia na uamuzi wa Rais kuanzisha wizara maalum ya kushughulikia masuala ya vijana, na kuongeza kuwa wao kama wazee wataendelea kutimiza wajibu wao wa kumshauri Rais pale inapohitajika.

Vilevile, amemshukuru Rais kwa hatua ya kuwapatia wazee bima ya afya ndani ya siku 10 za kwanza za utawala wake, akisema hatua hiyo itakuwa faraja kubwa kwa wazee. Pia amepongeza msaada wa magari mawili kwa ajili ya shughuli za Baraza la Wazee.

https://p.dw.com/p/54bWf
Ruka sehemu inayofuata TEC yakosekana sala ya kuombea mkutano wa Rais
2 Desemba 2025

TEC yakosekana sala ya kuombea mkutano wa Rais

Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) halikuwakilishwa katika dua ya kuombea mkutano wa hotuba ya Rais kwa Baraza la Wazee wa Dar es Salaam kama ilivyozoeleka. Badala yake, dua na sala ziliendeshwa na viongozi wa madhehebu mengine, wakiwemo kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), CCT na wengine.

Kwa muda sasa, TEC imekuwa katika mvutano wa wazi na serikali ya Rais Samia, ikiitoa lawama kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo utekaji na kupotea kwa baadhi ya wapinzani, pamoja na kuminywa kwa uhuru wa kisiasa.

Hivi karibuni, TEC ilitoa tamko kuhusu machafuko yaliyoshuhudiwa wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. Uchaguzi huo ulisusiwa na chama kikuu cha upinzani, Chadema, ambacho kiongozi wake, Tundu Lissu, anakabiliwa na kesi ya uhaini.

Katika tamko lake, TEC ilisisitiza kuwa amani ya nchi haiwezi kupatikana bila haki. Hata hivyo, baadhi ya watu waliikosoa kwa, kama walivyodai, kufumbia macho uharibifu uliofanywa na baadhi ya waandamanaji dhidi ya mali binafsi na za umma.

https://p.dw.com/p/54bQu
Ruka sehemu inayofuata Karibu kwenye blogu yetu mubashara
2 Desemba 2025

Karibu kwenye blogu yetu mubashara

Karibu kwenye blogu yetu leo Jumanne ambapo tunaangazi hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa Baraza la Wazee wa Dar es Salaam.

Mkutano huu unajiri katika wakati ambapo Tanzania inapitia wakati mgumu huku ikishuhudia mgawanyiko mkubwa kufuatia vurugu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Vurugu hizo zilizodumu kwa siku tatu zilisababisha mamia ya vifo na uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi, huku watu kadhaa wakishtakiwa kwa uhaifu, na miito ya kimataifa ikihanikiza kutaka kuheshimiwa kwa haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/54bLt
Onesha matokeo zaidi