Rais Goodluck Jonathan akutana na wazazi | Matukio ya Afrika | DW | 23.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais Goodluck Jonathan akutana na wazazi

Rais wa Naigeria Goodluck Jonathan amekutana kwa mara ya kwanza na wazazi wa wasichana zaidi ya 200 waliotekwa nyara na kundi la wanamgambo wa Boko Haram, na wasichana waliofanikiwa kukwepa kutekwa na wanamgambo hao.

Rais Jonathan na baadhi ya wasichana waliokwepa kutekwa

Rais Jonathan na baadhi ya wasichana waliokwepa kutekwa

Akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano na wazazi wa wasichana takriban 219 waliotekwa nyara Aprili 15, katika mji wa Chibok, Reuben Abati, msemaji wa serikali amesema rais Jonathan amewahakikishia wazazi kwamba wasichana wanaozuiliwa watarejea nyumbani wakiwa hai.

Abati amesema serikali ya shirikisho la Naigeria imeamua kufanya kila juhudi za kuwaokoa wasichana wanaozuiliwa na kuwajengea maisha mapya wasichana waliobakia mjini Chibok.

Rais wa Naigeria Goodluck Jonathan

Rais wa Naigeria Goodluck Jonathan

"Serikali itawaweka wasichana hawa katika shule nyengine, serikali itajenga upya mji wa Chibok, shule za upili na taasisi nyengine kwa hiyo wasichana hawapaswa kuwa na uwoga wowote," alisema Abati.

Hata hivyo nyuso za wazazi waliotoka katika mkutano huo hazikuonekana kuwa na matumaini yoyote ya kuwapata wasichana wao hivi karibuni.

Baada ya mkutano huo maafisa wa Usalama waliwazuwiya waandishi habari kuzungumza na wazazi hao.

Katika mkutano huo rais Goodluck Jonathan aliongozana na waziri wake wa Fedha na elimu pamoja na mshauri wake wa usalama wa taifa. Kashim Shettima Gavana wa jimbo la Borno pia alikuwepo katika mkutano huo uliofanyika jana jioni.

Shettima amewahi kumshutumu Jonathan kutofanya juhudi zaidi za kuwaokoa wasichana waliotekwa, pia aliikasirisha serikali kwa matamshi yake kwamba Wanamgambo wa Boko Harram wanasilaha zaidi kuliko jeshi la Naigeria.

Wazazi waliomba kukutana rais kwa muda mrefu

Kwa miezi kadhaa sasa wazazi wa wasichana hao wamekuwa wakiomba kukutana na rais Goodluck Jonathan, ombi lao lilikubaliwa baada ya mwanaharakati aliye na umri mdogo, raia wa Pakistan Malala Yousafzai kukutana na wazazi kisha baadaye na rais na kusisitiza umuhimu wa kuonana na kuzungumza na wazazi hao.

Nembo ya kampeni ya Bring Back Our Girls

Nembo ya kampeni ya Bring Back Our Girls

Kushindwa kwa serikali ya Naigeria kuwaokoa wasichana waliotekwa, kumesababisha kuanzishwa kampeni ya Kimataifa iliopewa jina la "BringBackOurGirls" yani warejeshe wasichana wetu huku kukiwa na maandamano ya mara kwa mara mjini Abuja kushinikiza hoja ya kuokolewa wasichana waliotekwa miezi mitatu iliopita.

Aidha wanamgambo wa Boko Haram wanasema ili kuachiwa kwa wasichana hao ni lazima serikali ya Naigeria iwaachie wapiganaji wake inaowazuilia jambo ambalo serikali bado haijaliridhia.

Baadhi ya wazazi waanza kufariki

Huku hayo yakiarifiwa wazazi 11 wa wasichana waliotekwa wameripotiwa kufariki, saba ambao ni wazazi wa kiume waliuwawa kutokana na shambulizi katika kijiji chao mapema mwezi huu huku wengine wanne wakifariki kutokana na magonjwa ambayo jamii ya Chibok inasema yametokana na kiwewe baada ya watoto wao kutekwa.

Kiongozi wa Jamii hiyo Pogu Bitrus amesema wazazi hao wamefariki kutokana na mshituko wa moyo, shinikizo la damu mwilini na magonjwa mengine.

Ramani ya mji wa Chibok walikotekwa wasichana

Ramani ya mji wa Chibok walikotekwa wasichana

Amesema baba mmoja wa wasichana hao alikosa fahamu na kubakia kulitaja jina la msichana wake hadi mauti yalipomkuta.

Kwa upande mwengine kundi la Boko Haram limeendelea kushambilia maeneo tofauti Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Wataalamu wanasema hujuma inayoendelezwa na kundi hilo inaonesha wazi wanaendelea kupanua mikakati yao tangu jeshi lilipofanikiwa kuwaondoa katika miji kadhaa katika jimbo la Borno.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP

Mhariri: Josephat Charo