Rais Bush ahutubia Knesset | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 15.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Rais Bush ahutubia Knesset

Rais Bush ashirikiana na waisraelö kusherehekea miaka 60 tangu kuundwa taifa hilo na wapalastina kwa upande wao wanaikumbuka "Nakba"-siku ya msiba

Rais Bush na waziri mkuu Olmert walipotembelea ngome ya Massada

Rais Bush na waziri mkuu Olmert walipotembelea ngome ya Massada


Rais George W. Bush wa Marekani amekaribishwa kwa shangwe na bunge la Israel Knesset,katika wakati ambapo wapalastina wanaadhimisha miaka 60 ya"Nakba",msiba wa kupotolewa na kwao.


Rais George W. Bush akifuatana na mkewe Laura alikaribishwa na spika wa bunge la Israel-Knesset,Dalia Yitzik.Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Marekani kuingia Knesset.


Akihutubia mbele ya wabunge wa Israel,rais George W. Bush ameelezea mafungamano ya dhati yaliyoko kati ya Marekani na Israel.

Rais Bush ameendelea kusema:


Marekani iko pamoja nanyi katika kuyavunja nguvu makundi ya kigaidi na kuwafungia njia wafuasi wa itikadi kali.Marekani iko pamoja nanyi kuvunja matumaini ya Iran ya kumiliki silaha za kinuklea.Kuwaruhusu wafadhili wakubwa wa ugaidi duniani kumiliki silaha za maangamizi ni jambo ambalo halitasamehewa na kizazi chochote kijacho.Kwa masilahi ya amani ,walimwengu hawastahili kuiachia Iran imiliki silaha za kinuklea."


Hotuba ya rais Bush haikudhukuru hata mara moja utaratibu wa amani kati ya Israel na Palastina.Hata hivyo waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert alizungumzia uwezekano wa kuidhinishwa na bunge makubaliano ya amani pindi yakifikiwa.


Katika wakati ambapo waisrael wanasherehekea miaka 60 ya kuundwa dola hiyo ya kiyahudi,wapalastina kwa upande wao wanamsiba,wakikumbuka siku wazee wao walipolazimishwa kuyapa kisogo maskani yao.Maandamano yamefanyika Ukingo wa magharibi na Gaza,wapalastina waliovalia nguo nyeusi wameongozana huku wakiimba nyimbo yao ya taifa-Biladi,Biladi"-


Huko Gaza wapalastina wakifuatana na wakuu wa chama cha Hamas wamekusanyika karibu na kivukio cha Erez wakilalamika dhidi ya vizuwizi walivyowekewa na Israel.

Jeshi la Israel limefyetua risasi hewani na kuvurumisha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao.


Maadhimisho ya Nakba yanafanyika katika wakati ambapo mazungumzo kati ya Israel na Palastina yaliyolengwa kufikia makubaliano ya amani kabla ya mwaka huu kumalizika,yanazorota.


""Usalama wa Israel unafungamana na uhuru na usalama wetu.Kuendelezwa uvamizi na Nakba hakutampatia usalama yeyote yule" amesema kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas katika hotuba yake hii leo.►◄

 • Tarehe 15.05.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E0QM
 • Tarehe 15.05.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E0QM
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com