1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila Odinga aendelea na mipango ya kuipinga serikali Kenya

Admin.WagnerD
16 Machi 2023

Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga ameongoza maandamano mjini Nakuru, ulio ngome ya mpinzani wake Rais William Ruto. huku viongozi wa mrengo huo wakitaka serikali kumuhakikishia kiongozi wao usalama.

https://p.dw.com/p/4OoFV
Kenia | Wahlkampf: Raila Oding
Picha: James Wakibia/Zuma/picture alliance

Kiongozi huyo wa muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja,  Raila Odinga amesema haogopi kuuwawa kwa ajili ya kuyatetea maslahi ya Wakenya. Raila vilevile ameapa kumshtaki Rais William Ruto kwa kuendelea kumchafulia jina na kumuhusisha na jaribio la mapinduzi ya serikali la mwaka 1982, na amesisitiza kuwa hana kesi ya kujibu.

Viongozi hao wamewarai Wakenya kujitokeza kwa wingi kwenye maandamano ya Jumatatu ijayo wakisisitiza kuwa yatakuwa ya amani.

Pamoja na hayo, wabunge wa muungano wa Azimio wamesisitiza kuwa siku ya Jumatatu ni siku ya mapumziko na wamewataka waajiri kuwapa ruhusa wafanyakazi wao ili waweze kuhudhuria maandamano hayo.

Rais Ruto atoa wito kwa Raila kuandaa maandamano ya amani

Aidha, wamemkosoa Naibu Rais, Rigathi Gachagua kwa matamshi yanayoonekana kuwatishia maisha viongozi wa azimio, na wamesema ni jukumu la polisi kuhakikisha usalama umeimarishwa siku hiyo.

"Iwapo Raila Odinga ataathiriwa kivyovyote siku ya Jumatatu, atakayewajibika ni Rigathi Gachagua na William Ruto,” alisema Seneta Edwin Sifuna.

Maandamano haya yamepingwa na baadhi ya wafanyabiashara na wadau wanaohofia huenda biashara zikasambaratishwa na hata wawezezaji kutoweka wakihofia vurugu.

Alikuwa akizunguma mjini Nakuru ambapo alijumuika na viongozi wengine wa mrengo wake wa Azimio la Umoja, katika mkutano wa umma ulioandaliwa siku moja baada ya kutangaza maandamano ya kitaifa, katika eneo linaloaminika kuwa ngome ya Rais William Ruto.

Mwandishi: Wakio Mbogho, DW, Nakuru.