Raia wateseka na mauaji, utekaji kaskazini mwa Msumbuji | Matukio ya Afrika | DW | 04.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Raia wateseka na mauaji, utekaji kaskazini mwa Msumbuji

Wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali wamekuwa wakivamia na kufanya vurugu kaskazini mwa Msumbiji. Lakini kutokana na sera ya habari inayominya upatikanaji wa taarifa, kumekuwa na maelezo kidogo kuhusu hali halisi.

Kwa saa kadhaa sasa, Biche Oliveira amesimama kwenye ufukwe wa kisiwa cha Quirimba, akiwatazama vijana wakishusha chakula kutoka kwenye mtumbwi. Idadi kubwa ya watu katika eneo hili wapo hapa kwa sababu wanapata chakula kinachogawiwa na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa mara moja kwa mwezi.

Muda mfupi kabla ya zamu yake, Oliveira anachomoa picha kutoka katika mfuko wa suruali yake akisema "Huyu hi binti yangu Muanarabo,". Ana miaka 16 na alitekwa nyara na wanamgambo wa Kiislamu walipovamia kisiwa. Waliwauwa wakaazi wawili, waliiba chakula na wakaichoma moto nyumba ya afisa mkuu wa utawala.

Soma pia: Amnesty yashutumu mauaji ya raia mzozo wa Msumbiji

Afisa wa utawala wa eneo hilo anathibitisha kuwa wakaazi 30 hawajulikani walipo, tangu shambulio lilipotokea na wengi waliopotea ni wasichana. Hizi ni habari ambazo bado watu wa nje ya kisiwa hicho kisicho na umeme wala huduma za simu hawajazisikia kwa takribani mwaka mmoja sasa.

Ankommen in Metuge, Hilfe für Mosambik

Raia wakikimbia kuokoa maisha kufuatia mwendelezo wa machafuko mkoani Cabo Delgado, Msumbiji.

"Hawa ni watu wabaya! wanatokea mbali, wanakuja hapa na kuwachukua watoto wetu bila kutueleza ni kwa nini na ni nini wanataka. Nina huzuni, nina hasira- Na wala sielewi ni kwa nini wanafanya hivi. Binti yangu alikuwa bado mwanafunzi. Alikuwa kwenye shule ya Kiislamu. Hata hakujua angependa kufanya kazi gani baadaye. Lakini alikuwa na ndoto za kuolewa na kuwa na watoto baadaye", anasema Biche Oliveira.

Issa Hamissi alishuhudia wakati Muanarabo alipotekwa nyara. Kijana huyu wa miaka 20, aliambiwa asali ili kuthibitisha kuwa ni Muislamu safi. "Walisema twende sote kambini kwetu. Tutakupa mafunzo ya namna kufyatua risasi na kukufanya uwe mpiganaji. Lakini mimi na vijana watano na wasichana wengine wawili tulipata namna ya kutoroka tukiwa njiani."

Hata hivyo, Munarabo hakuwa mmoja wao. Hamisi anakumbuka kuwa binti huyo alilia kwa huzuni huku wanaume waliowateka wakisema, tutawafanya kuwa wake zetu.

Mosambik | Moeda Cabo Delgado | Streitkräfte

Wanajeshi wa serikali ya Msumbiji wamenyooshewa kidole kwa kushiriki kuwatesa raia katika harakati zao za kupamba na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Ulinganisho na Boko Haramu

Jina la kundi linalodaiwa kuhusika na vurugu kaskazini mwa Msumbiji ni Al-Shabaab, ingawa halina uhusiano wowote na kundi la kigaidi la Somalia lenye jina kama hilo. Kuibuka na kuendelea kukua kwa ugaidi unaofanywa na kundi hilo lenye itikadi kali kunafanana na kundi la Boko Haram la Nigeria.

Walianzia kwenye maeneo yenye jamii zilizotengwa ambazo kwa muda mrefu zilipuuzwa na serikali. Wanasiasa na vikosi vya usalama vinapuuza itikadi kali kwa muda mrefu na kisha maafa yakitokea hujibu mapigo kwa kutumia nguvu kupitiliza, ikiwemo pia dhidi ya raia.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, lina rekodi za visa vinavyofanana na hiki. Shirika hilo liliwahoji watu 79 waliolazimika kuyakimbia makazi yao kati ya Septemba 2020 na Januari 2021 ambapo kulibainika uhalifu dhidi ya binadamu ukiwemo kunyongwa, kukatwa sehemu za mwili na kutekwa nyara kwa watoto wenye umri wa miaka saba.

Mosambik Binnenvertriebene aus Cabo Delgado

Mwanamke akiangalia nyumba yake iliyoharibiwa katika shambulio la magaidi katika mkoa wa Cabo Delgado.

Soma pia: Msumbiji yalaani ukatili wa mwanamke kuuawa, akiwa uchi

Dhumuni hasa la kundi hili haliko wazi na tangu mwaka 2019 limekuwa likijipambanua kama sehemu ya kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu. Eneo la Cabo Delgado linaloshambuliwa na kundi hili ni tajiri. Makampuni ya kigeni yanataka kuchimba gesi katika pwani yake. Hali ya usalama inachelewesha hili kufanyika na huenda serikali ikapoteza mapato muhimu.

Hadi sasa zaidi ya watu nusu milioni wamekimbia Cabo Delgado, na shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF linasema takribani nusu ya hao ni watoto.