″Putin havumilii misimamo mingine″ | Magazetini | DW | 26.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Putin havumilii misimamo mingine"

Kati ya mada nyingi zilizozingatiwa hii leo kwenye safu za wahariri wa magazeti ya Ujerumani, kwanza ni maoni kadhaa juu ya kuzuiliwa kwa waandamanaji wa upinzani nchini Urusi hapo jana.

Polisi iliwakamata waandamanaji wa upinzani mjini St. Petersburg

Polisi iliwakamata waandamanaji wa upinzani mjini St. Petersburg

Gazeti la “Rheinische Post” limechambua hivi juu ya kuzuiliwa na kukamatwa kwa wapinzani:


“Wiki moja kabla ya uchaguzi wa bunge, serikali ya Urusi ilisafisha barabara vizuri. Hatua kali ya polisi dhidi ya waandamanaji wa upinzani inalenga kumwonyesha kila mmoja kwamba Putin ndiye anayedhibiti mambo. Lakini kile ambacho hakieleweki ni kwa nini Putin ana hofu juu ya upinzani? Chama chake kwa hakika kitapata wingi wa kura, kwa sababu sheria mpya ya uchaguzi inahakikisha kwamba upinzani hauna nafasi yoyote. Hata hivyo, kukandamizwa kwao kunafichua shakashaka za serikali.”


Maoni mengine juu ya hali ya kisiasa nchini Urusi ni haya hapa ya mhariri wa “Flensburger Tageblatt”. Ameandika:


“Kama mfanyakazi wa zamani wa idara za ujasusi za Urusi, KGB, Putin havumilii misimamo mingine. Demokrasia yake inaelekea kuwa udikteta. Fedha za kugharamia polisi anazo kutoka mapato ya mafuta ambayo yanalipwa na nchi za Magharibi. Nchi hizo zinapaswa kutambua kwamba hazina ushawishi huko Urusi.”


Kwa mada nyingine tunaeleka Australia baada ya mpinzani Kevin Rudd kushinda uchaguzi. Kwa mujibu wa mhariri wa “Allgemeine Zeitung”, mabadiliko katika utawala wa nchi hiyo yataonekana zaidi kwenye sera za kimataifa kuliko ndani ya nchi. Katika uchambuzi tunasoma hivi:


“Mara tu ushindi wake ulipotanganzwa, waziri mkuu mpya Doland Rudd alisema wazi kwamba atawaondosha wanajeshi wa Australia kutoka Iraq. Kwa hivyo, Rais Bush wa Marekani atapoteza mshirika muhimu huko Iraq. Hata mambo yataweza kuwa mabaya zaidi kwa raisi wa Marekani, kwa sababu Kevin Rudd pia aliahidi serikali yake itatia saini makubaliano ya Kyoto kuhuzu utunzaji wa hali ya hewa. Hivyo, kwenye mkutano ujao wa Bali juu ya hali ya hewa utakaofanyika wiki ijayo, Bush atabakia peke yake anayekataa kutia saini makubaliano hayo ya kimataifa.”


Leo hii lakini, rais Bush wa Marekani ana shughuli nyingine, kwa vile ni mwenyeji wa mkutano wa kilele juu ya mustakabali wa Mashariki ya Kati huko Annapolis. Juu ya matumaini na matarajio kabla ya mkutano huu kuanza, mhariri wa “Nürnberger Zeitung” ameandika hivi:


“Wote wanaoshiriki hawana muda wa kuchelewesha zaidi juhudi za kutafuta amani. Rais Bush wa Marekani ambaye aliitisha mkutano huu anataka kipindi chake maradakani akimalize kwa mafanikio. Israel inahofia kwamba ikiwa mazungumzo hayatafanikiwa tena, makundi ya Kipalestina yenye msimamo mkali yataongeza shughuli zao. Rais Abbas wa Wapalestina atashindwa katika kinyang'anyiro juu ya mamlaka ya ndani iwapo mazungumzo yatashindwa. Nchi za Kiarabu zinazoshiriki kama vile Saudi Arabia na Syria zitapoteza ushawishi katika eneo zima la Mashariki ya Kati kama makubaliano hayatapatikana. Kwa hivyo, pande zote zina hamu kubwa kuleta mafanikio.”


 • Tarehe 26.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CTG4
 • Tarehe 26.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CTG4