1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin asifu mazungumzo ya Khazakhstan

27 Februari 2017

Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Syria yaliyofanyika Astana mwaka huu yamesaidia kufungua njia ya mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa mjini Geneva

https://p.dw.com/p/2YIsh
Wladimir Putin Russland Moskau
Picha: picture alliance/dpa

Awamu ya kwanza ya ya mazungumzo katika mji mkuu wa Khazakhstan, Astana yaliyofanyika mnamo mwezi Januari, Urusi na Iran ambao ni washirika wa Rais wa Syria, Bashar al-Assad na Uturuki ambaye ni mpinzani wa Assad, kwa pamoja walitiliana saini makubaliano tete ya kusitisha mapigano kati ya waasi na serikali ya Syria. 

Putin alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari alipofanya ziara nchini Khazakhstan kwamba "utaratibu  wa kusimamia mpango huo wa kusitisha mapigano umekwishaandaliwa, na hilo ndilo suala muhimu zaidi". Aliongeza kuwa huu ndio msingi uliofungua ukurasa wa kuanza upya kwa mazungumzo mjini Geneva. 

Makubaliano yaliyofikiwa Astana ya kusitisha mapigano yamekuwa yakivunjwa mara kwa mara, wakati ambapo vita dhidi ya makundi ya Jihadi, ambayo ni pamoja na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, ambalo halikuuhusishwa kwenye mpango huo huku vita vikiendelea kusambaa.
 
Hapo jana mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura alikutana na makundi mawili ya upinzani yanayoungwa mkono na Urusi, ambaye ni mshirika mkubwa wa Rais Assad. 

Syrien Krieg - Kämpfe in Daraa
Moshi ukifuka baada ya shambulizi kwenye eneo la Daraa nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/M. Abazeed

De Mistura aliieleza kamati kuu ya majadiliano ya amani nchini Syria, HNC inayowakilisha ujumbe wa upinzani kwamba angependelea kuyaunganisha makundi yaliyosambaratika ili kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na serikali ili kumaliza mzozo uliodumu kwa takriban miaka 6.

Jihadi Makdissi Kiongozi wa jukwaa la wapinzani wa walioko Cairo, aliwaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo kwamba wanataraji kismingi kuyaunganisha makundi yote ya upinzani ya nchini Syria ingawa alisema itakuwa vigumu kuyaunganisha makundi hayo kisiasa. 

Hamzi Menzer, kiongozi wa jukwaa la Urusi kwenye mazungumzo hayo, ambaye alikutana na mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa hapo jana amesema wamemwambia de Mistura juu ya haja ya kuyahusisha makundi yote katika mazungumzo hayo ya ana kwa ana.    

Menzer alitoa mwito pia wa kuungana kwa makundi hayo pinzani nchini Syria ili kuongeza ufanisi wa mazungumzo hayo.

De Mistura anataraji kukutana na wajumbe wa kamati kuu ya makubaliano ya Syria baadae leo hii.  

Mwandishi: Lilian Mtono/Reuters/APE.
Mhariri: Yusuf Saumu