1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Presseschau: Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef    
18 Februari 2020

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya mpango wa nchi za Umoja wa Ulaya wa kuanzisha ulinzi wa pamoja kwenye pwani ya Libya ili kuhakikisha kwamba vikwazo vya silaha dhidi ya Libya vinatekelezwa.

https://p.dw.com/p/3XvBK
Deutschland Polizei schützt Moschee
Picha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

 Frankfurter Rundschau 

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Rundschau anasema katika zama hizi ambapo chama, kama cha AfD cha mrengo mkali wa kulia, kinachafua hewa ya kisiasa nchini Ujerumani, inapasa kuwa na matumaini ya kiasi fulani tu. Hata hivyo inafaa kusema kazi ya kuyamulika na kuyashinda makundi kama hayo ndiyo kwanza inaanza.

Süddeutsche

Mhariri wa Süddeutsche anatilia maanani kwamba kwa mara nyingine tena mtuhumiwa ni polisi aliyesimamishwa kazi na anafafanua kwa kusema siyo jambo la kushangaza kwamba Waislamu nchini Ujerumani wamepoteza imani. Hata hivyo serikali inalo jukumu la kuwalinda Waislamu wanaohisi kutishiwa na makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia. Hata kama polisi hawatakuwa na uwezo wa kuilinda misikiti yote nchini Ujerumani, ni wajibu wa viongozi kutoa ishara zitakazowapa imani Waislamu. Sababu ni kwamba Waislamu, sawa na wananchi wengine nchini Ujerumani wana haki ya kupewa usalama. Pamoja na hayo, serikali na jamii yote kwa jumla inapaswa kuwa macho dhidi ya wale wanaochukia uislamu.

Tagesspiegel

Mhariri wa la gazeti la Tagesspiegel anatoa maoni juu ya mpango wa nchi za Umoja wa Ulaya wa kuanzisha ulinzi wa pamoja kwenye pwani ya Libya ili kuhakikisha kwamba vikwazo vya silaha dhidi ya nchi hiyo, anasema hatua hiyo inaelekea kwenye lengo sahihi lakini haitakuwa njia ya kuaminika sana katika kuzuia silaha kupelekwa pande zinazopigana nchini Libya. Jambo muhimu ni kwa nchi za magharibi kuacha kuziuzia silaha zile nchi  zinazopeleka silaha kwa pande zinazoziunga mkono nchini Libya. Ujumbe huo unaihusu hasa Ujerumani ambayo mwaka jana ilikubali kuuza nje silaha thamani ya Euro zaidi ya bilioni 1.3

Stuttgarter

Naye mhariri wa gazeti la Stuttgarter anaupongeza Umoja wa Ulaya kwa uamuzi wa kuanzisha mpango wa kuzuia silaha kuingia nchini Libya hasa baada ya kufanyika mkutano juu ya mgogoro wa Libya ambao haukuleta mafanikio makubwa. Gazeti hilo linaeleza kwamba baada ya nchi za Umoja wa Ulaya kuupitisha mpango wa  kuhakikisha vikwazo vinatekelezwa, hatua nyingi muhimu zinapaswa kuchukuliwa. Kwanza kudhibiti njia za ndani ya Libya zinazomwezesha jenerali Haftar kujipatia silaha. Pili kuziwekea vikwazo nchi zinazojiingiza katika mambo ya Libya na hivyo kusababisha nchi hiyo izidi kudidimia katika vurumai. Nchi za Umoja wa Ulaya zinahitaji kuwa na ujasiri wa kuchukua hatua hizo.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen