1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yavunja maandamano Harare

Kalyango Siraj27 Oktoba 2008

Waandanaji walitaka ufumbuzi wa haraka wa mkwamo wa kisiasa

https://p.dw.com/p/FiIH
Polisi wa ZimbabwePicha: AP

Polisi ya mjini Harare yawakamata wandamanaji wakati viongozi wa kanda ya kusini mwa Afrika SADC wanakutana tena kwa mazungumzo yenye nia ya kuunusuru mpango wa kugawana madaraka kati ya chama rais Robert Mugabe cha ZANU PF na cha mpinzani wake mkuu cha Movement for Democratic Change MDC cha Morgen Tsvangirai.Mpango huo umekwama kutokana na ugawanaji wa wizara muhimu.

Wahusika wakuu katika mgogoro wa Zimbabwe,rais Mugabe, waziri mkuu mteule, Morgen Tsvangirai na naibu wake Arthur Mutambara pamoja na mpatanishi wao Thabo Mbeki wanahudhuria mkutano huo.

Karibu wote hao isipokuwa Mbeki hawakusema lolote kwa waandishi habari wakati walipowasili katika hoteli walikokutana.

Bw Mbeki alisema kuwa anamatumaini kuwa mkutano huo wa kikanda utaweza kuyanusuru makubaliano ya kugawana madaraka ya Septemba 15.

Katika mpango wa awali wa kugawana madaraka,MDC cha Tsvangirai kilipewa wizara 13, kile cha Mutambara wizara 3 na ZANU -PF cha Mugabe wizara 15.Hata hivyo kizungumkuti kikawa makubaliano hayakufafanua ni wizara ipi itachukuliwa na chama gani.

Mambo yalizidi kuchacha baada ya Mugabe kukipa chama chake wizara zinazosemekana kuwa ni muhimu kama vile ya Ulinzi,mambo ya ndani pamoja na ya fedha jambo lililopingwa na Tsvangirai.

Kama ishara ya kutokubaliana na hatua hiyo,wiki iliopita alisusia mkutano wa kilelele wa jumuiya ya SADC uliofanyika Swaziland,yeye akitoa sababu kuwa alipewa hati ya kusafiria dakika za mwisho.Lakini pembeni wanachama wa MDC faraghani wanasema chama hakikupendelea ripoti ilioandaliwa na Mbeki wanaoiona kama yenye upendeleo.

Mugabe majuzi alitishia kuunda serikali yake mwenyewe ikiwa chama cha Tsvangirai hakitabadilisha msimamo wake kuhusu mgao wa wizara.Mbali na MDC kutaka kudhibiti wa wizara ya mambo ya ndani lakini pia msemaji wake Chamisa amesema pia kuwa hilo sio suala pekee lakini pia suala la wizara takriban 10.La sivyo Tsvangirai alionya kuwa atajiondoa.

Na kwa upande wake chama cha Mugabe cha ZANU -PF,kinamlaumu Tsvangirai kwa kuchukua madaraka kwa nguvu badala ya kuyagawana na pia kutaka kuyakwamisha ili kuuigiza Umoja wa Mataifa.

Wachambuzi wa masuala ya kisaisa wanasema kuwa ingawa pande mbili kuu katika mgogoro huo zinawajibika ili kuwaondolea usumbufu wananchi wa Zimbabwe lakini Tsvangirai anaonekana kama anawajibika sana wakati huu .

Mwenyekiti wa kundi linalojitegemea la National Constitutional Assembly-Lovemore Madhuku,ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa japo mapatano haya ni kugawana sawa lakini,katika mkutano wa jumatatu Tsvangirai anaweza akashinikizwa zaidi.Hii ni kutokana na imani ya viongozi wengi wa SADC kuwa Mugabe amesharidhia mengi.

Yeye mchambuzi mkongwe wa masuala ya kisiasa na mkosoaji mkuu wa Mugabe, John Makumbe,amesema mapema jumatatu kuwa mkutano huo ungeshindwa kufikia lengo ikiwa viongozi wa SADC watachukua msimamo wao wa kawaida wa kuwa nyuma ya Mugabe.

Kwa muda huohuo takriban watu 50 wamekamatwa mjini Harare.Wanaharakati wanasema waliokamatwa walikuwa wakijaribu kuandamana mbele ya hoteli ya mazungumzo ya kugawana madaraka.

Taarifa zaidi zinasema kuwa miongoni mwa waliokamatwa walikuwa wanafunzi pamoja na akina mama.Inasemekana wote hao walikuwa wanataka kufikiwa muafaka haraka ili hali ya maisha iboreshwe na pia shule ziweze kuanza tena baada ya kufungwa kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayiokabili nchi hiyo yaliyosababishwa na mgogoro wa kisiasa.