1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yathibitisha kuwapa ulinzi maafisa wa uchaguzi Kenya

2 Agosti 2017

Idara ya polisi imethibitisha kuwa maafisa wa tume ya uchaguzi watapewa ulinzi wa ziada zikiwa zimesalia siku 5 kabla uchaguzi mkuu kufanyika

https://p.dw.com/p/2hYsB
Kenia Wahlen EU Beobachter
Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Wasiwasi huo umeelezwa wakati ambapo idara ya polisi imethibitisha kuwa maafisa wa tume ya uchaguzi watapewa ulinzi wa ziada zikiwa zimesalia siku 5 kabla uchaguzi mkuu kufanyika. Wakati huohuo waangalizi wa jumuiya ya COMESA wamewasili nchini Kenya kabla uchaguzi mkuu wa tarehe nane wiki ijayo. Kutoka Nairobi Thelma Mwadzaya anaaraifu Zaidi.))

Ujjumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya ulioko nchini Kenya unatiwa wasiwasi na usalama wa maafisa wa tume ya uchaguzi ya IEBC zikiwa zimepita siku chache tangu mkurugenzi wa teknolojia na mawasiliano kuuawa eneo la Muguga katika kaunti ya Kiambu.Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya Marietje Schaake ametoa wito wa kuwapa ulinzi kamili wanaosimamia uchaguzi mkuu kwa misingi ya katiba ya nchi. Kauli hizo zinaungwa mkono na Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinett aliyeweka bayana kuwa maafisa wa tume ya uchaguzi watapewa ulinzi kamili. Hapo awali Rais Uhuru Kenyatta aliamuru maafisa wa tume ya uchaguzi kulindwa muda wote.

Usalama wa maafisa wa tume ya uchaguzi Kenya

Wanadiplomasia wa kigeni nao pia wanashinikiza kuwa ulinzi wa maafisa wa tume ya uchaguzi uimarishwe wakati ambapo uchunguzi wa mauaji ya Mkurugenzi wa teknolojia na mawasiliano Chris Msando unaendelea. Balozi wa Uingereza Nic Hailey na mwenzake wa Marekani Robert Godec pia wamelaani mauaji hayo. Lakini jee, kipi kinakubalika kisheria iwapo kiongozi wa ngazi ya juu wa tume ya uchaguzi atafariki dunia kabla siku ya uchaguzi? Joy Mdivo ni mwanasheria na afisa mkuu mtendaji wa kituo cha sharia cha EACLJ na anaelezea

Wakati huohuo waangalizi wa COMESA wamewasili nchini kabla uchaguzi mkuu kufanyika mnamo tarehe 8. Kikosi hicho kina wawakilishi wa Congo, Misri, Eritrea, Malawi,Sudan,Uganda, Zambia,Zimbabwe na sekretariati ya COMESA yenyewe.Ujumbe huu unaongozwa na Waziri wa Sheria wa Zimbabwe Balozi Simbi Mubako.kikosi hicho kitakutana na wadau pamoja na IEBC na waandishi wa habari kabla tarehe 8 mwezi huu na kitaoa taarifa yake rasmi baada ya uchaguzi mkuu kufanyika.Msemaji mkuu wa polisi nchini Kenya Charles Owino anaelezea mikakati ya usalama kwa jumla wakati wa uchaguzi mkuu.

Maafisa wa IEBC wamepewa walinzi wa ziada kufuatia mauaji ya mwenzao Chris Msando.Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Wafula Chebukati ameongezewa walinzi na magari ya usalama. Kadhalika maafisa wengine wa ngazi ya juu wamepewa maafisa 2 wa ziada wa ulinzi. Kutoka Nairobi mimi ni Thelma Mwadzaya.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya, DW - Nairobi
Mhariri: Iddi Ssessanga