1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi 25 wa Misri wauawa na wanamgambo

Admin.WagnerD19 Agosti 2013

Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye silaha wamewauwa maafisa 25 wa polisi nchini Misri, katika mashambulizi ya kuvizia asubuhi leo katika eneo la Sinai, na kivuko cha Rahah katika eneo hilo kimefungwa

https://p.dw.com/p/19S5Q
Wanajeshi wa Misri wakifanya doria katika eneo la Sinai
Wanajeshi wa Misri wakifanya doria katika eneo la SinaiPicha: Reuters

Katika mashambulizi hayo, wanamgambo wenye silaha waliyalazimisha kusimama mabasi mawili yaliyokuwa yakiwasafirisha maafisa hao wa polisi, na kuwalazimisha waliokuwemo kutoka nje na kulala chini, kisha wakawauwa mmoja mmoja kwa kuwapiga risasi.

Afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema polisi hao walikuwa wamevaa nguo za kiraia. Taarifa za hivi karibuni kabisa zinaeleza kuwa baada ya mashambulizi hayo, Misri imekifunga kivuko cha Rafah.

Mwendelezo wa umwagaji damu

Mauaji ya polisi hao ambayo yamefanyika karibu na kivuko hicho kilicho katika eneo la Sinai, yametokea siku moja baada ya tukio jingine la umwagaji damu mjini Cairo jana, ambapo polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi na kuwauwa wafuasi 36 wa rais aliyepinduliwa Mohamed Mursi. Polisi inadai kwamba wafuasi hao walikuwa wamemshika mateka mlinzi wao ndani ya gari walimokuwa wamefungiwa. Vifo hivyo vya jana na leo vimeifanya idadi ya watu waliokwishauawa tangu Jumatano iliyopita kufika takribani 1,000.

Wafuasi wa Mursi waliokamatwa wakisafirishwa kwenda gerezani
Wafuasi wa Mursi waliokamatwa wakisafirishwa kwenda gerezaniPicha: Reuters

Wafungwa waliouawa jana walikuwa katika malori ya magereza, ambayo yalikuwa katika msafara yakiwahamishia katika gereza la Abu Zaabal kaskazini mwa mji mkuu, Cairo. Katika msafara huo walikuwemo wafungwa 600 waliokamatwa katika maandamano ya kupinga kupinduliwa kwa Mohamed Mursi.

Afisa wa usalama aliliambia shirika la habari la Associated Press kuwa wafungwa katika lori mojawapo walizusha fujo na kumpiga vibaya mlinzi, hali ambayo iliwafanya polisi kuingilia kati na kufukiza gesi ya kutoa machozi ndani ya lori hilo.Baadhi ya taarifa zilisema kuwa wafungwa hao walikufa kwa kukosa pumzi, na nyingine zilieleza kuwa walipigwa risasi walipokuwa wakijaribu kutoroka.

Al-Sisi ashikilia uzi ule ule

Akizungumza na maafiusa wa jeshi jana, Kamanda mkuu wa jeshi la Misri Jenerali Abdel Fattah al-Sisi, alisisitiza kuwa jeshi litakuwa na msimamo shupavu dhidi dhidi ya ghasia, lakini pia akatoa wito wa kujumuishwa kwa wafuasi wa Mursi katika mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo.

''Tutawahudumia kwa nia njema Wamisri wote wanaodhamiria mazuri. Kwa wale watakaokwenda kinyume cha hayo, hatutakuwa na chaguo jingine bali kukabiliana nao.'' Amesema Jenerali al-Sisi.

Mara tu baada ya mauaji dhidi ya polisi asubuhi ya leo, zilijitokeza taarifa zinazopingana juu ya namna mauaji yalivyofanywa. Awali ilielezwa kuwa mabasi waliyokuwa wakisafiria yalishambuliwa kwa maguruneti ya kurushwa kwa roketi.

Jenerali Abdel Fattah al-Sisi, kamanda mkuu wa jeshi la Misri
Jenerali Abdel Fattah al-Sisi, kamanda mkuu wa jeshi la MisriPicha: Reuters

Sinai ni eneo nyeti kiusalama ambalo linapakana na Israel pamoja na Ukanda wa Gaza, na limekuwa likishuhudia mashambulizi ya karibu kila siku tangu kupinduliwa kwa rais Mohamed Mursi tarehe 3 Julai mwaka huu.

Jana mamia ya wafuasi wengi wa Mohamed Mursi walikamatwa nchini Misri, baada ya msako uliofanywa katika nyumba zao. Baraza la mawaziri pia limefanya kikao cha dharura, kutafakari uwezekano wa kulipiga marufuku kundi la udugu wa kiislamu.

Hata hivyo, kundi hilo bado halionyeshi dalili zozote za kusalimu amri na kuachana na madai yake ya kutaka kiongozi wao Mohamed Mursi arejeshwe madarakani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef