1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland na Hungary zaukosoa uamuazi wa mahakama ya Ulaya

Amina Mjahid
16 Februari 2022

Poland na Hungary zimeghadhabishwa na uamuzi wa Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya wa kutupilia mbali pingamizi lao la kikwazo kipya cha kuondoa ufadhili kwa nchi wanachama wanaokiuka uhuru na haki za kidemokrasia.

https://p.dw.com/p/477ZU
 Ursula von der Leyen
Picha: Virginia Mayo/AP/picture alliance

Waziri wa Sheria wa Hungary Judit Varga kupitia ujumbe aliouandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter ameutaja uamuzi huo kama "uliochochewa kisiasa" na "ushahidi hai kwamba Umoja wa Ulaya unatumia vibaya madaraka yake."

Hungary inasema inaadhibiwa kutokana na sheria tata kuhusu wapenzi wa jinsia moja iliyoipitisha mwaka jana.

Naye Waziri wa Sheria wa Poland Zbigniew Ziobro amesema Umoja wa Ulaya unaelekea kuwa chombo ambacho nguvu inaweza kutumika kuwanyima na kubana uhuru wa nchi wanachama.

Uamuzi huo uliotolewa na mahakama hiyo iliyoko Luxembourg unamuwekea shinikizo Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen kufanya uamuzi wa iwapo na ni lini ataanza kuutekeleza.