1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pigo kwa Trump baada ya Matt Bevin kushindwa Kentucky

6 Novemba 2019

Chama cha Democratic kimeibuka na ushindi katika uchaguzi wa gavana katika jimbo la Kentucky, licha ya Rais wa Marekani Donald Trump kumfanyia kampeni mgombea wa chama cha Republican Matt Bevin. Andy Beshear alishinda.

https://p.dw.com/p/3SXrN
Andy Beshear
Picha: Getty Images/J. Sommers II

Chama cha Democratic kimeibuka na ushindi katika uchaguzi wa gavana katika jimbo la Kentucky, licha ya Rais wa Marekani Donald Trump kumfanyia kampeni mgombea wa chama cha Republican Matt Bevin. Andy Beshear alishinda na kuchukua udhibiti wa eneo hilo huku ikibainika wazi kuwa hoja ya kupambana na trump katika maeneo ya vitongojini inaendelea.

Matokeo ya uchaguzi wa Jumanne katika majimbo manne ambayo yanajumuisha Kentucky, Virginia, Mississippi na New Jersey, yameanza kutoa dalili jinsi gani uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani utakavyokuwa, wakati Trump akiwa analenga kuwania tena urais kwa muhula wa pili wa miaka minne.

Mwanasheria mkuu wa chama cha Democraitc Andy Beshear alipata ushindi mwembamba dhidi ya Gavana Matt Bevin licha ya kufanya mkutano wa kampeni usiku wa kuamkia uchaguzi akipigiwa debe na Rais Trump.

Akizungumza baada ya ushindi huo Andy Beshear amesema  “wapiga kura wa Kentucky wametuma ujumbe wa wazi kabisa kwa kila mtu ausikie. Ni ujumbe kwamba chaguzi zetu hazitakiwi tu kuhusu mashindano kati ya mrengo wa kulia na mrengo wa kushoto. Chaguzi zetu bado zinahusu mambo yaliyo sahihi na yasiyo sahihi. "

Soma zaidi:Mzozo wa Wademocrat na Trump wachacha

Trump ambaye alishinda Kentucky kwa asilimia 30 katika uchaguzi wa mwaka 2016  katika mkutano huo aliwaambia wapiga kura kwamba walihitaji kumchagua tena Bevin, kwa sababu wapinzani wake watasema "Trump ataweka historia ya kushindwa vibaya zaidi katika historia ya dunia" kauli ambayo imedhihirika baada ya Bevin kushindwa.

Huku matokeo hayo yakionekana kuwa pigo kwa rais Trump, ambaye bado ni maarufu Kentucky, huenda yametokana na kushuka kwa umaarufu wa Bevin jimboni humo, matokeo ya uchunguzi wa maoni yamebainisha kuwa Bevin huenda akawa gavana ambaye umaarufu wake umeporomoka sana kufikia kiwango cha chini kabisa Marekani baada ya kujiingiza katika malumbano na mivutano na vyama vya wafanyakazi na waalimu.

Mwanasheria mkuu Gordon Sondland amekabidhiwa ushahidi mwengine

Gordon Sondland
Picha: Public Domain

Wakati haya yakiarifiwa, mwanadiplomasia Gordon Sondland amekabidhi ushahidi mwingine kwa wachunguzi wanaotaka rais Trump afunguliwe mashtaka. Sondland amekiri kile ambacho wabunge wa chama cha Democratic wanasema ni njama ya kubadilisha ushahidi, kutokana na shinikizio la Trump na wakili wake Rudy Giuliani na Ukraine. Sondland amesema msaada wa kijeshi kwa Ukraine unazuiliwa mpaka rais wa Ukraine atakapokubali kutoa taarifa kuhusu kupambana na rushwa kama Trump alivyotaka.

Rais Trump amekanusha madai ya kubadilisha ushahidi lakini wabunge wa chama cha Democratic wanasema kuna msimamo mmoja unaojitokeza tangu mawasiliano yake ya simu mnamo Julai 25 mwaka huu na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, wakati alipoomba msaada maalum. Ombi hilo ambalo lilijumuisha uchunguzi dhidi ya makamu wa rais wa zamani Joe Biden pamoja na mtoto wake, ndilo lililoanzisha mchakato wa kutaka kumchunguza na kumfungulia mashitaka Trump.

RTRE/AP