1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Paredi la ubingwa lasimamisha shughuli mjini Leverkusen

27 Mei 2024

Wachezaji na mashabiki wa Bayer Leverkusen wamesherehekea katika mitaa mbalimbali mjini Leverkusen mwishoni mwa juma baada ya kuchukua ubingwa wa ligi kuu soka Ujerumani Bundesliga na Kombe la Shirikisho DFB-Pokal.

https://p.dw.com/p/4gLXs
Wachezaji wa Bayer Leverkusen wakisherehekea mbele ya mashabiki baada ya kuifunga FC Kaiserslautern kwenye fainali ya DFB-pokal
Wachezaji wa Bayer Leverkusen wakisherehekea mbele ya mashabiki baada ya kuifunga FC Kaiserslautern kwenye fainali ya DFB-pokal Picha: Federico Gambarini/dpa/picture alliance

Maelfu ya mashabiki waliojawa na furaha walimiminika barabarani, huku baadhi yao wakifanikiwa kuligusa Kombe la DFB-pokal, walipoungana na vijana wa Xabi Alonso wakati wa msafara na shamrashamra za kusherehekea ubingwa.

"Binafsi, nimefarijika mno hasa baada ya kuwa shabiki wa Leverkusen tangu mwaka 1988 na kila wakati tukisubiri kushinda kombe. Na sasa, hatimaye hilo limetokea. Tunajivunia," ameeleza mmoja wa mashabiki wa Leverkusen.

Kilele za sherehe hizo zilifanyika katika uwanja wao wa nyumbani Bay Arena.

Soma pia: Alonso ahisi fahari na uchungu baada ya 'Neverlusen' kushindwa

Kocha wa Bayer Leverkusen Xabi Alonso amesema, "Najivua sana kuwa na wachezaji na mashabiki hawa. Wajua, siamini kama msimu umekamilika, msimu huu umekuwa kama ndoto. Hali imekuwa nzuri  mpaka siku ya mwisho, ni kitu cha kufurahia, nguvu waliotupa mashabiki katika uwanja huu. Nafurahi sana kuwa na kikosi imara kama hiki."

Bayer Leverkusen ilimaliza msimu wa Bundesliga bila ya kupoteza mechi hata moja kwa kujikusanyia alama 90 na kumaliza alama 17 mbele ya Stuttgart iliyomaliza katika nafasi ya pili na Bayern Munich, ambao ni mabingwa kwa misimu 11 iliyopita, ilitulia katika nafasi ya tatu.