1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na Haki

Papa Francis: Naelewa upinzani wa kubariki ushoga Afrika

1 Februari 2024

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amesema anaelewa upinzani unaoshuhudiwa miongoni mwa makasisi wa Afrika kuhusu kubariki wapenzi wa jinsia moja, akisema "ushoga" unachukuliwa kuwa "mbaya" barani humo.

https://p.dw.com/p/4bwL9
Vatikan, Italia | Papa Francis akisalimiana na wageni
Papa Francis akisalimiana na wageni wake waliomtembele VatikanPicha: VATICAN MEDIA / ipa-agency.net/picture alliance

Katika mahojiano yaliyochapishwa siku ya Jumatatu (29.01.2024), Papa Francis amesema anaamini kuwa siku moja pendekezo lake la kuwabariki wapenzi wa jinsia moja litaeleweka vyema ispokuwa barani Afrika ambako amesema hilo ni "suala nyeti na lisilovumilika" kwa Waafrika kutokana na misimamo yao ya kitamaduni.

Papa Francis ameliambia Gazeti la Italia "La Stampa" kwamba wale wanaopinga vikali wazo hilo ni kundi la maaskofu wachache wa kihafidhina huku akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kujumuisha na sio kugawanya.

Soma pia:Mamia ya Waislamu waandamana Kenya kupinga ushoga

Amesisitiza kuwa hajali kuhusu hatari ya maaskofu hao wahafidhina kujitenga na Kanisa Katoliki kutokana na tamko hilo akitaja kuwa ni vyema kuangalia mbele.

Tamko la kuwabariki wapenzi wa jinsia moja lilitolewa mwezi uliopita katika waraka unaofahamika kama Fiducia Supplians na kusababisha mjadala mkubwa katika Kanisa Katoliki, na hasa upinzani mkali kutoka kwa maaskofu wa Afrika.

Ni ipi sera hiyo mpya ya Vatican?

Papa Francis aliifanyia mabadiliko ya kihistoria sera ya Vatican kwa kuruhusu makasisi kuwabariki wapenzi wa jinsia moja wanaotafuta neema ya Mungu katika maisha yao.

Vatikan Italia | Papa Francis
Papa Francis akiwa katika huduma mjini VatikanPicha: GUGLIELMO MANGIAPANE/REUTERS

Lakini sera hiyo inasisitiza kuwa Maaskofu wanaweza wasibariki mahusiano ya watu wa jinsia moja.

Lakini sera hiyo imesisitiza kuhusu uamuzi usiobadilika wa"sakramenti ya ndoa" ambayo ni lazima iwe kati ya mwanaume na mwanamke na kwamba baraka za wapenzi wa jinsia moja zisilinganshwe hata kidogo na taratibu za ndoa.

Soma pia:Benki ya Dunia yakemea sheria ya Uganda dhidi ya mashoga

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amesisitiza kwamba wakati baraka hizo zinatolewa, mapadre wanapaswa kwanza kuzingatia muktadha, hisia na mahali wanakoishi watu hao na kutathmini njia zinazofaa zaidi kulifanikisha hilo.

Kwa nini tamko hilo lina utata barani Afrika?

Tamko hilo limezua mtafaruku ndani ya Kanisa Katoliki, hasa kutoka kwa maaskofu wa bara la Afrika, ambako kuna waumini wa kikatoliki wapatao milioni 265 ikiwa ni sawa na karibu robo ya Wakatoliki bilioni 1.3 duniani kote.

Waumini hao wanaishi na makanisa yao yanafanya kazi katika jamii ambazo ushoga unalaaniwa na kuharamishwa.

Museveni aitetea sheria ya kupinga ushoga

Kulingana na Shirika la kutetea haki za mashoga (LGBTQ+) la Human Dignity Trust, jumla ya nchi 31 kati ya 54 kote Afrika, zina sheria zinazoharamisha ushoga, ikiwa ni zaidi ya bara lingine lolote duniani.

Soma pia:Papa ashutumu ushoga kufanywa uhalifu

Mwezi Januari, maaskofu wa Kikatoliki kutoka Afrika na hususan visiwani Madagascar walitoa taarifa ya pamoja wakikataa kufuata sera hiyo mpya ya kuwabariki wapenzi wa jinsia moja na kudai kwamba mahusiano kama hayo “ni kinyume na matakwa ya Mungu.”

Taarifa hiyo, iliyotiwa saini na Kadinali Fridolin Ambongo wa Kongo kwa niaba ya makongamano ya kitaifa ya maaskofu wa Afrika, ilionyesha kwa uwazi zaidi pingamizi la bara zima la Afrika kuhusu tamko hilo.