Papa Francis awaosha miguu wafungwa | Masuala ya Jamii | DW | 30.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Papa Francis awaosha miguu wafungwa

Katika salamu zake za Pasaka, Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, ameosha na kuibusu miguu ya wafungwa kwenye ibada ya Alhamis Tukufu katika jela ya Regina Coeli ya mjini Roma. 

Miongoni mwa wafungwa waliokoshwa miguu na Papa Francis wamo Waislamu wawili, Mkristo wa madhehebu ya Orthodox na muumini mmoja wa Buddha, ikiwa ni mara nyengine kwa Papa huyo kuchaguwa kuadhimisha Alhamis Tukufu akiwa na wale waliopatwa na matatizo maishani.

"Kila mtu daima ana fursa ya kubadilika kimaisha na hakuna mwenye haki ya kumuhukumu," alisema Papa Francis kwenye jela hiyo ya wanaume watupu.

Hii ni mara ya nne ndani ya miaka mitano ya uongozi wake kwa Papa kuadhimisha siku hii tukufu kwa Wakristo kwenye jela za Italia.

"Kwangu, kuwatembelea wagonjwa, kwenda gerezani, kuwafanya wafungwa kuhisi kuwa wana matumaini ya kurekebishika tabia zao, hayo ndiyo mahubiri ya Kanisa," alisema kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki katika kitabu chake cha hivi karibuni cha mahojiano.

Mwaka huu, wafungwa 12 walikoshwa miguu yao na Papa Francis wakitokea kwenye mataifa ya Italia, Ufilipino, Morocco, Colombia, Moldova, Sierra Leone na Nigeria. 

Mila ya zamani

Mila hii, inayofanywa kila mwaka kwenye siku ifahamikayo kama Maundy au Alhamis Tukufu, inaadhimisha Chakula cha Mwisho cha Jioni cha Yesu Kristo na wanafunzi wake.

Italien Vatikan Papst Franziskus Messe Osterdonnerstag (Reuters/S. Rellandini)

Papa Francis akiogoza Ibada ya Alhamis Tukufu

Kwenye mapokeo ya Kikristo, inasemwa kuwa Yesu aliwakosha miguu yao kabla ya mlo huo kuashiria imani yake kwao.

"Mimi nina madhambi kama nyinyi, lakini leo namuwakilisha Yesu Kristo... Mungu kamwe hatuwachi mkono, kamwe hachoki kutusamehe," Papa Francis aliwaambia wafungwa hao.

Sherehe hii ni sehemu ya maadhimisho ya Pasaka kuelekea Jumapili ya Pasaka.

Tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013, Papa huyo ameondosha ile mila ya kuwaosha watu miguu kutoka ndani ya Vatican na kuielekeza kwa watu wenye matatizo au wanaotengwa na jamii.

Katika mwaka wake wa kwanza, alitembelea jela ya vijana ambako alitekeleza mila hiyo kwa kundi la wafungwa vijana, wawili wao wakiwa Waislamu, akiwa kiongozi wa kwanza wa Kanisa Katoliki kufanya hivyo.

Mwaka 2014, alikosha miguu ya vikongwe na watu wenye ulemavu, ambapo mwaka 2015 alifanya hivyo kwenye jela moja na mwaka uliofuatia akachaguwa kituo cha kuwapokea wahamiaji.

Siku ya Ijumaa Njema, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani atawaongoza waumini kukumbuka mateso na kifo cha Kristo.

Kilele cha Sikukuu ya Pasaka ni misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Roma siku ya Jumapili, ambapo Papa Francis atagawa baraka za Urbi na Orbi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Zainab Aziz

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com