Papa Francis ahimiza msamaha kwa waasi wa Colombia | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Papa Francis ahimiza msamaha kwa waasi wa Colombia

Papa Francis Ijumaa hii atalitembelea eneo lililowahi kuzingirwa na waasi wa mrengo mkali wa kushoto, na kushiriki ibada pamoja na wahanga wa mzozo wa muda mrefu nchini Colombia huku akiwataka kuwasamehe wauaji hao. 

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis Ijumaa hii(08.09.2017) atalitembelea eneo ambalo liliwahi kuzingirwa na waasi wa mrengo mkali wa kushoto, ambako huko atashiriki ibada pamoja na wahanga wa mzozo uliodumu kwa muda mrefu nchini Colombia na kuwataka kuzishinda huzuni zao kwa kuwasamehe wauaji hao wa zamani. 

Masuala muhimu ya ziara yake kwenye mji wa Villavicencio ni ile ambayo Wavatican wanaitaja kama "kusanyiko kubwa la sala kwa ajili ya maridhiano ya kitaifa". Linatarajiwa kuwa ni kusanyiko la majonzi makuu kwa Papa Francis, ambaye amelifanya suala la maridhiano kuwa lengo maalumu la ziara yake ya siku tano nchini Colombia baada ya ahadi yake ya kulitembelea taifa hilo, kufuatia kutwa saini kwa makubaliano ya amani kati ya serikali na Colombia na waasi wa kundi la FARC.

Tukio hilo litahudhuriwa na maelfu ya wahanga kutoka kada mbalimbali, kuanzia wanajeshi waliopoteza viungo vyao vya mwili wakati wakifukua mabomu ya kuchimbiwa ardhini, kina mama ambao watoto wao walipatiwa mafunzo kinguvu na waasi ambao hawakuweza kuwaona tena na wakulima walioondolewa kutoka kwenye ardhi zao na makundi haramu ya kijeshi ya mrengo wa kulia.

Kolumbien Papst Franziskus in Bogota (Reuters/O. Romano)

Papa Francis katika ibada iliyofanyika katika mji mkuu wa Colombia, Bogota.

Waasi hao wa zamani wanatarajiwa pia kuhudhuria, lakini waratibu wa tukio hilo kutoka Vatican na Colombia hawajaonyesha dalili yoyote kuhusu iwapo uongozi wa FARC utakuwepo, ama hata kukutana na Papa wakati wa ziara yake, hatua inayoonyesha inaweza kutonesha upya majeraha ya mzozo na kuamsha upya hisia kali zinazoweza kuchochewa na wapiganaji hao wa zamani wa msituni kujitokeza mbele ya hadhara ambao bado wanachukiwa na idadi kubwa ya watu.

Hapo Jana Papa Francis katika ibada iliyofanyika katika mji mkuu wa Colombia Bogota, aliwahimiza Wacolombia kukabiliana na huzuni zao zilizosababishwa na vita vya kutisha vilivyodumu kwa miaka 50, lakini pia aliwataka viongozi kuandaa sheria itakayomaliza uvunjwaji wa sheria na kutokuwepo kwa usawa wa kijamii ambao huzalisha mbegu za machafuko.

Miongoni mwa watakaohudhuria ni Lucresia Valencia, ambaye alimpoteza mume na mtoto, lakini pia alipoteza mkono wake wa kulia na mguu wa kushoto wakati walipokuwa wanaelekea kutafuta kuni karibu na makaazi yao. Mji aliokuwa akiishi kwa miaka mingi uligubikwa na machafuko na anasema, anataka dunia itambue kwamba amani ya taifa hilo bado ni tete. Amesema, mabomu ya kufukiwa ardhini yaliyomuharibia maisha yake mwaka 2009, yalidhaniwa kuwa yalitegwa na kundi jingine la waasi la National Liberation Army, ELN, ambalo bado liko hai katika maeneo mengi nchini humo.

Kolumbien Aktion Opfer von Staatsgewalt (DW/C. Esguerra)

Baadhi ya familia za wahanga wa mzozo wa Colombia pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu waliokusanyika mjini Bogota

Zaidi ya ibada hii, kutakuwa ni sanamu ya Kristu iliyoharibiwa na kuokolewa kwenye kanisa lililoshambuliwa na bomu miaka 15 iliyopita, na ambayo labda inaweza kuwa ni ukumbusho wenye nguvu zaidi wa machafuko mabaya ya kisiasa ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 250,000 na mamilioni kuyakimbia makazi yao. Baadhi ya Wakolombia waliochanganyika na Waafrika walioishi kwenye mji ulioharibiwa wa Bojaya walisafiri kwa siku kadhaa kwa boti, ndege na basi kuiwasilisha sanamu hiyo Villavicencio, ili kubarikiwa na Papa Francis.

Sanamu hiyo ilikuwa kwenye kanisa ambalo lililishambuliwa kwa kuharibiwa kabisa na waasi wa FARC wakati ambapo raia 300 walikuwa wamejificha kulipoibuka mashambulizi ya risasi yaliyohusisha makundi ya waasi, wanajeshi na makundi haramu ya kijeshi. Kiasi ya raia 79 walikufa na wengine 100 kujeruhiwa katika shambulizi hilo mwaka 2002.

Leo hii mji huo ulioko mbali ni alama ya upatanisho, ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia mpango wa amani wa Rais wa nchi hiyo Juan Manuel Santos, na hata kuchukua hatua ambayo si ya kawaida ya kuwakaribisha tena waasi wa FARC, ambao viongozi wao kwa mara mbili tofauti wameutembelea mji huo kuomba msamaha  na kuanzisha miradi inayonufaisha jamii ya hapo.

Mapema kwenye ibada hiyo, Papa Francis atawataja watakatifu mapadre wawili ambao walitambulika zaidi kwenye mzozo huo wa Colombia, ambao Papa alisema waliuwawa kutokana na chuki dhidi ya imani yao.  

Mwandishi: Lilian Mtono
Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com