1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa alazimika kuendesha Misa ya Pasaka kwa mtandao

12 Aprili 2020

Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani amelazimika kuvunja mila ya karne kadhaa ya ibada ya Jumapili ya Pasaka kwa kuiendesha misa hiyo kwa njia ya mtandao badala ya kukaa na waumini kutokana na khofu ya kirusi cha corona.

https://p.dw.com/p/3anDW
Italien | Coronavirus | Papst Franziskus Betet den Kreuzweg ohne Pilger
Picha: Getty Images/AFP/V. Pinto

Akiendesha ibada hiyo siku ya Jumapili (Aprili 12), ambayo mtu pekee aliyekuwa mbele yake alikuwa mpigapicha wake, Papa Francis alitoa wito kwa walimwengu kutokukubali kutawaliwa na khofu katika wakati huu dunia inapopambana na ugonjwa wa COVID-19, na badala yake watambuwe kuwa "giza na mauti sivyo vyenye kauli ya mwisho."

"Kwa wiki kadha sasa, tumeendelea kurejelea kauli kwama 'mambo yatakaa sawa,' tukijiambatanisha kwenye uzuri wa ubinaadamu na kuruhusu maneno ya kutia moyo kusimama kwenye nyoyo zetu. Lakini kadiri siku zinavyokatika na khofu kuongezeka, ndivyo ambavyo hata wale majasiri kabisa wanavyoweza kujikuta wakivunjika moyo. Tusitamauke.... Tunaweza na lazima tuwe na matumaini," alisema mkuu huyo wa Kanisa Katoliki akiwa kwenye maktaba yake binafsi ndani ya Kanisa la Mtakatifu Petro. 

Kauli ya Papa Francis ilipongezwa na Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte, kwa kile alichosema ni ishara yake ya uwajibikaji kwa kuadhimisha Pasaka akiwa faragha.

"Licha ya kuwa maneno yake yametamkwa mbali kutoka Uwanja wa Mtakatifu Petro, ambao kwa sasa umefunikwa na kimya cha kutisha, yamemfikia kila mtu," alisema waziri mkuu huyo wa taifa ambalo lenyewe limeshuhudia vifo vya makumi kwa maelfu ya watu.

Ibada hiyo inayowajumuisha pamoja waumini bilioni 1.3 wa Kanisa hilo ulimwenguni inawakilisha kufufuka kwa Yesu Kristo, ambapo waumini mjini Rome walijaza keki mashuhuri za Pasaka siku kadhaa kabla, kuadhimisha sikukuu yao muhimu.

Pasaka ya upweke na kujitenga

Vatikan Papst eröffnet Osterfeierlichkeiten
Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis.Picha: Getty Images/AFP/A. Di Meo

Siku ya Ijumaa Kuu, Papa Francis alifika kwenye uwanja mtupu wa Vatican akiwa amevalia joho lake jeupe ili kuuwasha mwenge wa kuashiria mwanzo wa ibada, lakini baadaye kiongozi huyo mwenye asili ya Argentina na mwenye umri wa miaka 83 alikiri kwamba hata yeye mwenyewe anajihisi kwamba ni kama vile ametiwa "tunduni."

Kwa zaidi ya miaka 50, tukio hili lilikuwa likifanyika mbele ya hadhara ya watu wasiopunguwa 20,000, lakini tangu mwanzoni mwa Machi mji wa Rome, kama yalivyo mengine ya Italia, umekuwa kwenye zuio na kujitenga kutokana na athari za kirusi cha corona.

Misa ya Jumapili ya Pasaka na kile kinachoitwa ujumbe wa baraka wa "Urbi et Orbi" vilihuhudhuriwa na watu 70,000 mwaka jana kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro. Lakini kwa sasa lango la kuingilia makao makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, limefungwa na linalindwa na polisi wenye silaha waliovalia vifaa vya kujikinga na maambukizi nyusoni na mikononi mwao.

Kwenye mahojiano yake yaliyochapishwa na magazeti kadhaa ya Kikatoliki, Papa Francis alikiri wazi kwamba hata yeye anapambana kama mtu mwengine yeyote ili kukifanya kipindi hiki kiwe na maana maishani mwake. "Tunapaswa kuishughulikia hali hii kwa kujitenga tukiwa na ubunifu. Ama tunaweza kupata mfadhaiko na kutengwa au tunaweza kuwa wabunifu zaidi."