Pakistan kuwanyonga wanamgambo 500 | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Pakistan kuwanyonga wanamgambo 500

Pakistan inapanga kuwanyonga kiasi cha wanamgambo 500 ndani ya wiki chache zijazo, baada ya serikali kuondoa marufuku ya muda ya kutumika adhabu ya kifo dhidi ya wanaotiwa hatiani kwa ugaidi.

Watoto wa skuli wakishiriki sala ya kuwaombea wenzao waliouawa na Taliban, Jumanne iliyopita.

Watoto wa skuli wakishiriki sala ya kuwaombea wenzao waliouawa na Taliban, Jumanne iliyopita.

Afisa mmoja wa ngazi za juu kwenye wizara ya mambo ya ndani ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wizara yake tayari imeshakamilisha kesi za watuhumiwa hao 500, ambao maombi yao ya msamaha yametupiliwa mbali na rais na kwamba watanyongwa ndani ya wiki chache kutoka sasa.

Vikosi vya polisi na jeshi vimetumwa kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na viwanja vya ndege na magereza yamewekwa kwenye hali ya tahadhari kutokana na hatua hiyo ya unyongaji, na huku jeshi likiimarisha operesheni yake dhidi ya Taliban.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Chaudhry Nisar Ali Khan, alisema wamepokea taarifa kwamba Taliban inapanga mashambulizi zaidi kufuatia kunyongwa kwa wapiganaji wake.

"Baada ya tukio hili na baada ya kunyongwa kwa magaidi, na pia kwa sababu ya operesheni ambazo wanajeshi wetu wanazifanya kwenye eneo la kaskazini magharibi, tumepokea taarifa za kiintelijensia kote nchini kwamba wanamgambo wanajitayarisha kufanya mashambulizi mengine ya kinyama. Sote tunapaswa kuwa na tahadhari ya hali ya juu," alisema Chaudhry.

Waziri Mkuu Nawaz Sharif amemuamuru mwendesha mashitaka mkuu wa serikali kuhakikisha kesi zote dhidi ya washukiwa wa ugaidi zilizoko mahakamani zinaendeshwa kwa haraka.

Tayari 6 wameshanyongwa

Muombolezaji wa mashambulizi ya kigaidi ya Peshawar.

Muombolezaji wa mashambulizi ya kigaidi ya Peshawar.

Kutokea siku ya Ijumaa hadi sasa, wanamgambo sita tayari wameshanyongwa, katika kile kinachoonekana kuwa na jibu la serikali kwa ghadhabu za wananchi baada ya Taliban kuwauwa watu 149, miongoni mwao watoto 133 katika mji wa Peshawar.

Miongoni mwa wanamgambo sita waliokwishanyongwa, watano walitiwa hatiani kwa kushiriki njama ya kumuua aliyekuwa rais wa Pakistan, Jerenali Parvez Musharraf, mwaka 2003, ambapo mmoja alitiwa hatiani kwa kuhusika na mashambulizi dhidi ya makao makuu ya jeshi mwaka 2009.

Kwa mujibu wa naibu mkuu wa magereza wa Pakistan, Sikandar Khan Kakar, takribani washukiwa 100 huenda wakanyongwa mapema zaidi, wakiwemo 14 ambao Rais Manmoon Hussain, amewakatalia msamaha.

Wapiganaji wawili wa ngazi za juu wa Taliban, Mohammed Aqeel na Arshad Mehmood, walikuwa wa mwanzo kunyongwa siku ya Ijumaa mjini Faisalabad, siku mbili baada ya Waziri Mkuu Sharif kutangaza kufutwa kwa marufuku ya kutumika adhabu ya kifo dhidi ya watuhumiwa wa ugaidi.

Pakistan imeyaelezea mashambulizi ya Jumanne dhidi ya skuli ya kijeshi kama ndiyo mashambulizi ya Septemba 11 dhidi yake, na kusema kuwa yamebadili sura nzima ya vita vyake dhidi ya makundi yenye siasa kali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com