Othman Masoud: Makamo wa kwanza wa rais Zanzibar | Matukio ya Afrika | DW | 01.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Othman Masoud: Makamo wa kwanza wa rais Zanzibar

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amemteuwa Othman Masoud Othman kushika wadhifa wa makamo wa kwanza wa rais, baada ya kifo cha aliyekuwa makamo wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.

Baada ya kusubiri kwa siku kadhaa kuzibwa nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki Feb 17, mwaka huu, hatimaye nafasi hiyo imejazwa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said imesema uteuzi huo umeanza leo ikiwa ni takwa la kikatiba chini ya kifungu cha 9 (3) cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. 

Kitaaluma Othman Masoud ni mwanasheria na ametumikia serikali tokea kipindi cha kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi akianzia na Dk Salmin Amour Juma, baadae alifanya kazi na Dk Amani Karume mwaka 2000 hadi 2010 akishika nafasi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, baadae aliteuliwa kushirika nafasi ya Mwanasheria mkuu wa serikali katika kipindi cha Dk Ali Mohammed Shein.

Lakini kabla ya kumaliza kipindi cha uongozi wake Dk Shein cha miaka mitano mwaka 2014 aliondoshwa kwenye wadhifa huo kutokana na msimamo wake wa kuitetea Zanzibar ndani ya Muungano wakati wa majadiliano na mchakato wa kupitisha katiba mpya ya Tanzania.

Soma zaidi: Othman Masoud ndiye makamu wa kwanza mpya wa rais Zanzibar

"Kwa kweli tumefurahi sana uteuzi wa Othman Masoud kwasababu huyu ni mwanasheria nguli, ni mtu mwenye hekima, ni mtu mwenye busara na mtu mwenye maono ya mbali sana na kwa kweli tumpongeze sana Dk Hussein Mwinyi kwa kukubali uteuzi huu kwasababu yule ndiye atakayefuata hasa hatua za Marehemu maalim seif kwa sababu ya suala la kushirikisha watu kwa pamoja," alisema Suleiman Seif Omar mhadhiri wa chuo kikuu cha Zanzibar na mchambuzi wa masuala ya kitaifa na kimataifa anaishi visiwani Zanzibar

Uteuzi wa Othman kuwa makamu wa kwanza wa Rais umefanyika baada ya majadiliano mazito kuhusu ni nani angefaa kuvaa kiatu cha Maalim Seif Sharif Hamad.

Sherehe za kumuapishwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar zitafanyika kesho Saa nne Ikulu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, viongozi wa dini na wananchi.

Mwandishi: Salma Said