Operesheni dhidi ya IS yaongeza chuki dhidi ya Ulaya | Matukio ya Afrika | DW | 20.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Operesheni dhidi ya IS yaongeza chuki dhidi ya Ulaya

Warusha ndege wa zamani wa Marekani wameiambia serikali yao kuwa ndege zinazoruka bila ya rubani kwa nia ya kuwaangamiza waasi wa Dola la Kiislamu yanasababisha kuongezeka kwa chuki dhidi ya nchi za Magharibi.

Katika barua yao ya wazi kwa Rais Barack Obama, Waziri wa ulinzi Ashton Carter na mkurugenzi wa CIA John Brennan, warusha ndege hao wanne, Brandon Bryan, Cian Westmoreland, Stephen Lewis na Michael Haas wametoa wito wa kutaka kufanyika upya kwa tathmini juu ya matumizi ya ndege hizo sizizo na rubani.

Sehemu ya barua hiyo ilisema "hatuwezi kukaa kimya na kushuhudia majanga kama vile mashambulizi ya paris huku tukijua kuhusu athari zinazotokana na mpango wa matumizi ya kushambulia kwa kutumia ndege hizo huko nje na hapa nyumbani."

Wapiganaji wa kundi la kigaidi Dola la Kiislamu

Wapiganaji wa kundi la kigaidi Dola la Kiislamu

Warusha ndege hao wa zamani walisema mara nyingi ndege hizo zisizo na rubani kwa bahati mbaya zimekuwa zikishambulia hata wale wasio walengwa katika operesheni hiyo na kupelekea ndugu wa wanaouawa kuwaona kuwa ni waoga na matokeo yake mara nyingi wale wanaoepuka mashambulizi hayo hutaka kulipiza kizazi dhidi ya mataifa ya magharibi kutokana na kile wanachookita mauaji ya wasio na hatia.

"Tuligundua kuwa kufuatia kuuawa kwa raia wasio na hatia kumepelekea kuwapo kwa hisia za chuki ambazo hupelekea mwamko wa ugaidi na kuwepo makundi kama vile dola la kiislamu kupata nafasi,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Matatizo ya kisaikolojia

Baada ya kuendesha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwa miaka 20, mashambulizi ambayo pia hupelekea mauaji ya watu wasiona na hatia, kundi hilo la wastaafu lilisema wanataabika na matatizo ya kisaikolojia yanayotokana na msongo wa mawazo na kiwewe au Post Traumatic Stress Disorder (PTSD), suala linalopelekea wengi wao kuingia katika tatizo la ulevi kupindukia na matumizi ya dawa kupita kiasi ikiwa ni matokea ya kiwewe.

Kiongozi wa ndege zisizokuwa na rubani

Kiongozi wa ndege zisizokuwa na rubani

Mmoja wa wastaafu hao, Michael Haas alisema “Kazi hii si sawa na michezo ya video, unapokosea kulenga na kumuuua mtu ambaye si mlengwa huwezi kusema uanze tena upya.” Aliyekuwa mrusha ndege mwandamizi mstaafu, ambaye pia alitumika kutoa mafunzo kwa marubani wengine wa kimarekani alisema, waongozaji wengi wa ndege hizo wamekuwa wameingiwa ganzi na mashambulizi hayo ya kutumia ndege.

Obama ametilia nguvu zaidi mpango wa mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani tangu alipoingia madarakani mwaka 2009 na ameruhusu zaidi aina hiyo ya mashambulizi ikilinganishwa na rais aliyepita George Bush.

Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la "The Intercept" mwezi Oktoba, idadi ya watu wasio na hatia wanaouawa katika mashambulizi hayo ya ndege ni kubwa ukilinganisha na idadi inayotolewa na ikulu ya Marekani.

Mwandishi: Mwazarau Mathola/ dw/ksb/bw (Reuters, AFP)

Mhariri: Saumu Mwasimba

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com