Obama na Karzai kukutana | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama na Karzai kukutana

Kikao cha viongozi hao kitajadili mustakabali wa Afghanistan hasa katika uwezo wake wa kukabiliana na kitisho cha ukosefu wa usalama baada ya kuondoka jeshi la NATO mwaka 2014.

Rais Barack Obama na mwenzake wa Afghanistan Hamid Karzai mwaka 2012 Kabul

Rais Barack Obama na mwenzake wa Afghanistan Hamid Karzai mwaka 2012 Kabul

Rais Barack Obama wa Marekani leo (Ijumaa) tarehe 11.01.2013 anakutana na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan katika ikulu ya Marekani kujadiliana mustakabali wa Afghanistan hasa katika uwezo wake wa kukabiliana na kitisho cha ukosefu wa usalama. Mkutano huo unakuja baada ya hapo jana rais huyo wa Afghanistan kukutana na waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta.

Mazungumzo kati ya viongozi hao yanatarajiwa kuchukua muda wa masaa mawili katika Ikulu na baade wawili hao watakula pamoja chakula cha mchana kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Leone Panetta und rais Hamid Karzai

Waziri wa ulinzi wa Marekani Leone Panetta und rais Hamid Karzai

Wasiwasi wa usalama

Mkutano huu unafanyika katika kipindi kigumu wakati Rais Obama akikusudia kuyaondoa majeshi yake ambayo ni sehemu ya jeshi la Jumuiya ya Kujihami ya NATO lililokuwa na jukumu la kutoa mafunzo, kupambana na magaidi pamoja na kuliunga mkono jeshi la Afghanistan kuhakikisha kundi la kigaidi la al-Qaida halirudi tena katika nchi hiyo ya Afghanistan wakati NATO imeondoa majeshi yake mwaka 2014.

Siku ya Alhamisi Rais Karzai alikutana na waziri wa ulinzi Leone Pannetta ambaye aliweka wazi kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili utaendelea kuwa imara na kwamba hatua kubwa zimepigwa kufuatia mazungumzo yao na juu ya hilo akaongeza kusema,

''Baada ya kupita kipindi kirefu na kigumu hatimae naamini juu ya ukurasa wa mwisho wa kuundwa Afghanistan yenye kujitegemea ambayo inaweza kusimamia mambo yake na usalama wake kwa ajili ya mustakali wake''

Matumaini

Rais Karzai amepata matumaini kwamba serikali yake na ya Marekani zitaweza kukubaliana juu suala la usalama.

"Afghanistan itaweza kuwahakikishia usalama watu wake na kuilinda mipaka yake kwa msaada utakaotolewa," amesema rais huyo ambaye baadae alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa katika wizara ya mambo ya ulinzi ya Marekani na waziri wa mambo ya nje, Hillary Clinton.

Jeshi la Marekani nchini Afghanistan

Jeshi la Marekani nchini Afghanistan

Rais Karzai kimsingi anaunga mkono hatua ya kubakia wanajeshi wachache wa Marekani baada ya mpango wa kuondoka kwa jeshi la NATO mwaka 2014, lakini yote itategemea kitakachofikiwa katika mkataba kuhusu usalama ambao bado unajadiliwa, mkataba ambao utasimamia masuala kama kupewa kinga za kisheria wanajeshi wa Marekani pamoja na kuhamishwa wafungwa katika jela za Afghanistan.

Hata hivyo itakumbukwa kwamba utawala wa Rais Obama ulishindwa kufikia mwafaka wa mpango kama huo kwa ajili ya Iraq baada ya vita hatua iliyomfanya Rais Obama kuwarudisha wanajeshi wake wote nyumbani.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com