Obama aahidi kushirikiana na Republican | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama aahidi kushirikiana na Republican

Rais Barack Obama ameahidi kushirikiana na wabunge wa Republican baada ya ushindi wao mkubwa kwenye uchaguzi, ingawa ameonya kuna mambo atayafanya bila ya wao kulinda ajenda zake za msingi.

Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari usiku wa jana, kiongozi huyo wa Marekani amekaribia kukubali dhamana ya moja kwa moja kwa kushindwa vibaya kwa chama chake cha Democrat mikononi mwa wapinzani wao, ambao wamefanikiwa kuugeuza uchaguzi huo kuwa lipizo la kisasi dhidi ya sera zake.

Hata hivyo, amewahakikishia Wamarekani kwamba bado yuko imara na sauti yao ameisikia: "Nikiwa rais, nina wajibu wa pekee katika kujaribu na kuufanya mji huu ufanye kazi. Hivyo, kwa kila mmoja wenu aliyepiga kura, ninataka mujuwe kuwa nimewasikieni. Kwa thuluthi mbili ya wapiga kura mulioamua kutokupiga kura zenu, nimewasikieni pia. Sote tunapaswa kuwapa Wamerekani sababu ya kujihisi kwamba mahala waliposimamia ni imara."

Sasa Republican wanaongoza baraza la Seneti, wameongeza nguvu zao kwenye Baraza la Wawakilishi na wameshinda ugavana kwenye maeneo ambayo awali yalitawaliwa na Democrat. Chama cha Republican kinaamini kuwa wapiga kura wamemuadhibu Obama kwa kuwa wanapingana na sera zake za ndani na za nje.

Kiongozi wa walio wengi kwenye Seneti, Mitch McConnell.

Kiongozi wa walio wengi kwenye Seneti, Mitch McConnell.

"Tutakuwa na idadi kubwa kabisa ya mabaraza ya Republican na viti kwenye mabunge ya majimbo kuwahi kupatikana kwenye historia. Huu ulikuwa ushindi wa aina yake. Na yote haya yaliyotokana na kukataliwa moja kwa moja kwa ajenda ya Obama," alisema Reince Priebus, mwenyekiti wa kamati kuu ya chama hicho.

Muelekeo mpya wa Republican

Viongozi wawili wa juu wa Republican bungeni, Spika John Boehmer na kiongozi wa walio wengi kwenye Seneti Mitch McConnell, walisema chombo hicho sasa kitajikita kwenye uundaji wa nafasi mpya za ajira na uchumi.

Hata hivyo, suala kubwa ambalo watakumbana nalo ni kuyageuza mafanikio ya Obama kwenye sera yake ya bima ya afya, maarufu kama Obamacare, ambayo imewanufaisha mamilioni ya Wamarekani masikini.

Kwa pamoja, pande zote mbili zimeonesha ishara ya kushirikiana kwenye masuala muhimu ya nchi likiwemo la kupitishwa kwa sera ya mageuzi kwenye kodi na kutatuwa mikwamo katika mikataba ya biashara za kimataifa.

Obama aliwaambia waandishi wa habari usiku wa jana katika ikulu ya White House, kwamba ataliomba bunge kuidhinisha ajenda yake ya kupambana na Ebola, lakini akaonya kwamba katika masuala mengine, kama vile mageuzi kwenye sheria za uhamiaji, hatasubiri maridhiano na bunge asilokuwa na nguvu nalo, na badala yake atatumia nguvu zake "kama rais kuhakikisha mageuzi yanafanyika."

Mwandishi: Mohammed Khelef/APAFP
Mhariri: Saumu Yussuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com