Njia ya Brexit inaanza kufunguliwa na Scoxit ikifuatia | Magazetini | DW | 29.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Njia ya Brexit inaanza kufunguliwa na Scoxit ikifuatia

Brexit na malumbano kama Uingereza ilipe au la kitita cha Euro bilioni 60 kwa Umoja wa Ulaya, Scoxit, baada ya bunge la Scotland kuunga mkono pendekezo la kuitishwa kura ya maoni kujitenga na Uingereza magazetini

Tunaanzia njia panda inayoiunganisha Uingereza na Umoja wa ulaya. Njia hiyo itafungwa, kutokana na maombi ya Uingereza ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya-Brexit-hatua inayotarajiwa kukamilika miaka miwili kutoka sasa. Masuala ya fedha yamegeuka kuwa mzizi wa fitina katika malumbano yatakayoanza baada ya waziri mkuu Theresa May kuwasilisha maombi hayo leo mjini Brussels. Gazeti linalosomwa na wengi humu nchini "Bild" linahimiza kila la kufanya lifanywe kuepusha mfarakano. Gazeti linaendelea kuandika: "Brexit itakapowadia, na kila kitu kinaonyesha itawaadia, hakuna anaeweza kuashiria madhara ya aina gani yatatokea. Ndio maana ni muhimu kufanya kila liwezekanalo kuepusha madhara yasiwe makubwa-kwa Ujerumani, kwa Umoja wa Ulaya na kwa Uingereza pia! Kwa sababu kila mmoja ataendelea kumhitaji mwenzake, kiuchumi, katika sera za usalama na pia kiutamaduni. Ndio, inatisha jinsi serikali ya Uingereza ilivyowaongoza wananchi wake katika njia ya Brexit bila ya mipango. Lakini pia ni aibu jinsi sauti zinavyopazwa mjini Brussels kutaka waengereza wachukuliwe kama mfano, ili pasitokee yeyote mwengine atakaesubutu kuwaiga. Kile ambacho baadhi bado hawajakitambua ni kwamba Umoja wa Ulaya unabidi ujigeuze wenyewe kuwa kivutio kwa mataifa wanachama na wananchi wake na sio kwa vitisho."

 

Madhara yaepushwe

 Gazeti la kusini mwa Ujerumani "Stuttgarter Nachrichten" lina maoni sawa na hayo. Linakumbusha umuhimu wa mshikamano mnamo wakati huu unaoshuhudia mageuzi ya kimkakati nchini Marekani. Gazeti linaendelea kuandika: "Na hasa wakati huu ambapo rais wa Marekani Donald Trump anakosoa mtindo mmoja faida nono katika biashara ya nje ya Ujerumani, Ujerumani inauhitaji Umoja wa ulaya. Mgombea kiti cha rais kutoka Ufaransa anaepewa nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi, Emmanuel Macron anaonyesha tayari upepo utavumia upande gani. Anatishia kuichukulia hatua Marekani. Hilo linaweza kuzilinda shughuli za kiuchumi za Ufaransa lakini wakati huo huo kuitia katika mitihani mikubwa biashara  ya nje ya Ujerumani. Kwa hivyo diplomasia itakuwa na kazi kubwa ili masilahi ya Ujerumani yasiachwe kando, Uingereza itakapojitoa katika Umoja wa ulaya.

 

Scoxit itafuatia Brexit

Baada ya Brexit kuna Scoxit-kifupisho cha juhudi za Scotland za kutaka kujitenga na Uingereza. Bunge la mjini Edinburgh limeunga mkono pendekezo la kuitishwa kwa mara ya pili kura ya maoni katika Scotland yenye utawala wa ndani. Gazeti la "Der neue Tag" linaandika: Kishindo kinachomkabili waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ni kikubwa. Zimwi la mtengano waingereza waliloliita, linaendelea kumwandama. Scotland inataka kuitisha kura ya pili ya maoni mwaka 2019 kuamua kama wanataka uhuru kutoka Uingereza au la. Wascotland wanahisi madai yao hayakutiliwa maanani. Wanataka angalao waendelee kuwa mwanachama wa soko la pamoja-lakini waziri mkuu hatati kuisikia fikra hiyo. Zaidi ya hayo waziri mkuu huyo wa Uingereza anashikilia akihoji hataki kuzungumzia kuhusu Scoxit kabla ya Brexit kukamilika.

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Gakuba, Daniel