1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kuunda kikosi kipya mashariki mwa Ulaya

Admin.WagnerD11 Februari 2016

Mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wameidhinisha kikosi kipya cha kimataifa kuimarisha ulinzi katika nchi za mashariki ya Ulaya wanachama wa jumuiya hiyo ambazo zinatishiwa na Urusi

https://p.dw.com/p/1HtfU
Mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Brussels. (10.02.2016)
Mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Brussels. (10.02.2016)Picha: Reuters/Y. Herman

Katibu Mkuu wa Jumuiya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema Jumatano (10.02.2016) kikosi hicho kipya kitakuwa cha kimataifa na kitazunguka katika nchi wanachama za Ulaya ya mashariki badala ya kuwekewa kambi mahala pamoja.

Stolternberg ameweka wazi kwamba kwa NATO shambulio dhidi ya mshirika mmoja litakuwa sawa na shambulio kwa jumuiya nzima.

Amesema "Hiki kitakuwa ni kikosi cha kimataifa na ifahamike kabisa kwamba shambulio dhidi ya mshirika mmoja ni shambulio dhidi ya washirika wote na kwamba jumuiya nzima itajibu mapigo.Kikosi hicho kitakuwa cha kimataifa,kitazunguka na kitasaidiwa na mpango wa mazoezi na vifaa utakaorahisisha uwekaji wa vikosi vyake kwa haraka."

Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya NATO amesema wataalamu wa mipango ya kijeshi wataamua muundo wa kikosi hicho wakati kipindi cha machipuko.

Kikosi cha NATO kwa bahari ya Aegean

Uturuki na Ugiriki zimekubali kuiomba NATO kutuma kikosi cha kufuatilia wimbi la wakimbizi katika bahari ya Aegean na kupambana na magenge yanayosafirisha watu kwa magendo.

Wakimbizi katika bahari ya Aegean.
Wakimbizi katika bahari ya Aegean.Picha: picture-alliance/AA/B. Akay

Uturuki na Ugiriki zimeitaka NATO kutathmini hali hiyo kwa kutumia askari wa ulinzi wa mwambao wa taifa pamoja na idara ya ulinzi wa mipaka barani Ulaya Frontex.

Zikiwa mbioni kuzuwiya wakimbizi kumiminika Ugiriki licha ya kuwepo kwa makubaliano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya kudhibiti wimbi hilo la wakimbizi Ujerumani na Uturuki ziliwashangaza washirika wenzao wiki hii kwa kusema watalizusha suala hilo kwa jumuiya ya kujihami ya NATO.

Ushiriki wa Ujerumani

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula Von Der Leyen amesema Ujerumani iko tayari kushiriki katika kikosi kitakachoongozwa na NATO kufuatilia wakimbizi katika bahari ya Aegean.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von Der Leyen katika mkutano wa NATO mjini Brussels.(10.02.2016)
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von Der Leyen katika mkutano wa NATO mjini Brussels.(10.02.2016)Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/D. Aydemir

Amesema "Kwa hiyo ni vizuri kwamba Uturuki imeitaka NATO kuimarisha shughuli zake za uchunguzi katika bahari ya Aegean.Lengo lazima liwe kufanya iwe vigumu au isiwezekane kabisa kufanyika kwa biashara mbaya kabisa ya kusafirisha watu kwa magendo kwa kutumia uhamiaji haramu.Hilo litajadiliwa katika mkutano huu na Ujerumani iko tayari kushiriki katika shughuli hizo."

Umoja wa Ulaya umezidi kuishinikiza Ugiriki kuhusiana na suala hilo la mzozo wa wakimbizi barani Ulaya kwa kuitaka iboreshe mazingira ya wakimbizi na kuimarisha usalama wa mipaka yake venginevyo itazuiliwa kuwa mwanachama wa kanda yake ya kusafiri bila ya paspoti.

Umoja wa Ulaya umesema serikali ya Ugiriki inapaswa iwahudumie vizuri zaidi wakimbizi ili kwamba nchi zilizoelemewa na mzigo huo wa wakimbizi ziweze kuwarudisha wahamiaji katika nchi walikowasili kwanza Ugiriki kwa mujibu wa sheria za umoja huo wenye nchi wanachama 28.

Mwandishi ; Mohamed Dahman

AFP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman