Nani kuibuka kidedea leo Manchester United au Chelsea ? | Michezo | DW | 20.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Nani kuibuka kidedea leo Manchester United au Chelsea ?

Leo ndio ile siku iliokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa kabumbumbi sio tu barani Ulaya bali pia duniani kwa jumla wakati ndugu wawili wa Uingereza watakapokwaruzana kuwania ubingwa wa soka barani Ulaya.

default

Mchezaji wa kiungo wa Manchester United (katikati) Paul Scholes yumkini akawemo katika kikosi cha timu yake leo.

Mpambano huo wa fainali ya ligi ya vilabu bingwa Barani Ulaya unawakutanisha Manchester United ikijaribu kujishindia kwa mara ya tatu kombe hilo na Chelsea klabu ambayo iko mbioni kuandika historia yake yenyewe katika mpambano huo utakaofanyika katika uwanja wa Luzhniki mjini Moscow.

Fainali inayowakutanisha watoto wa Uingereza watupu imekuwepo kwa musa sasa baada ya timu hizo za ligi kuu ya Uingereza kufikia fainali tatu zilizopita za ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya na kufikia nusu fainali tatu mara tatu mwaka jana na safari hii.

Umilikaji wa kigeni,uwekezaji na wachezaji umeifanya ligi kuu ya Uingereza inufaike na utandawazi wa kandanda lakini kuna wengi katika mchezo huo wa soka wanaopiga chafya kutokana na kutamba kwa Uingereza kwa hivi sasa katika soka.

Lakini hayo sio ya kuwatia mashaka makocha Sir Alex Ferguson wa Machester United na Avram Grant wa Chelsea ambao wana mazingira na historia tafauti.

Ferguson ambaye kwa miaka 22 amekuwa akionowa United na kujishindia ubingwa kwa zaidi ya mara 24 akiwa kama kocha anajaribu bahati yake dhidi ya Grant ambaye amekuwa na mafanikio makubwa ya soka nchini Israel lakini ameanza tu kuifundisha Chelsea hapo mwezi wa Septemba mwaka jana.

Ferguson hivi sasa anajaribu kujishindia kwa mara ya pili ubingwa wa Ulaya baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani huko Barcelona hapo mwaka 1999.

Saleh Mcomoroh shabiki wa soka nchini Uingereza anaiwekea matumaini timu ya Chelsea kunyakuwa ubingwa huo.

Mpambano huo wa leo pia unakuja miaka 40 baada ya United kushinda mara ya kwanza klabu bingwa bara Ulaya na miaka 50 baada ya ajali ya ndege ya Munich ambayo imeuwa watu 23 wakiwemo wachezaji wanane wa United.

Kwa mujibu wa Ferguson changamoto kubwa kwa sasa ni kuamuwa nani wa kumuweka nje sio tu katika kikosi cha kwanza bali kwa wale wanaobakia ubaoni.

Hata hivyo inaonekana kama vile nafasi imetengwa kwa ajili mchezaji mkongwe wa kiungo Paul Scholes ambaye alifunga bao la ushindi dhidi ya Barcelona katika nusu fainali na kukosa fainali za mwaka 1999 kutokana na kufungiwa.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika fainali za Kombe la Chama cha Soka Uingereza hapo mwaka 1997 na Ferguson anakiri kwamba kushindwa na Chlesea katika mchezo huo bado kunauma.

Timu zote mbili hazina wasi wasi na suala la majeruhi na wachezaji wa Chelsea John Terry na Didier Drogba wanatazamiwa kujimwaga uwanjani baada ya kupona majeruhi.

Ushindi mjini Moscow sio utaipatia Chelsea ubingwa wao wa kwanza wa bara la Ulaya bali pia utamsaidia kocha wake Grant kuzima uvumi kwamba lazima ashinde ili kuhakikisha kwamba anaendelea kubakia na klabu hiyo.

Kocha huyo amekaririwa akisema kila pale unapoandika historia unataka historia hiyo iwe msingi wa kipindi cha usoni. Anasema wako furahani sana kwa katika fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya Chelsea lakini hawataki kuridhika na hilo tu.

Urusi imeruwahusu mashabiki wa Uingereza 40,000 wenye tiketi za halali kuingia nchini humo bila ya viza na takriban polisi na wanajeshi 6,000 wamewekwa tayari kwa ajili ya mechi hiyo na kuzuwiya fujo.

 • Tarehe 20.05.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E3H3
 • Tarehe 20.05.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E3H3
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com