1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atakuwa Waziri Mkuu mpya wa Italia?

Babu Abdalla28 Agosti 2019

Kiongozi wa mrengo wa kulia Matteo Salvini amepigiwa upatu kushinda wadhifa huo wa waziri mkuu. 

https://p.dw.com/p/3OdUk
Kiongozi wa mrengo wa kulia Matteo Salvini amepigiwa upatu kushinda wadhifa huo wa waziri mkuu. 
Kiongozi wa mrengo wa kulia Matteo Salvini amepigiwa upatu kushinda wadhifa huo wa waziri mkuu. Picha: picture-alliance/AP/ANSA/C. Peri

Hali ya kisiasa nchini Italia inazidi kutokota huku nchi hiyo ikitarajiwa kuwa na waziri mkuu mpya wakati wowote kutoka sasa. Kiongozi wa mrengo wa kulia Matteo Salvini amepigiwa upatu kushinda wadhifa huo wa waziri mkuu. 

Raia wa Italia wanasubiri kwa hamu kujua ni nani atakayechukua wadhifa wa waziri mkuu mpya nchini humo.

Kwa mujibu wa afisa mkuu wa chama cha Democratic Party, PD, ni kuwa chama hicho kimefanya mazungumzo ya dakika za mwisho na vuguvugu la nyota tano (M5S) kwa ajili ya kuanzisha serikali mpya na pia kuepuka uchaguzi wa mapema huku kiongozi mfuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia Matteo Salvini akipigiwa upatu  kushinda.

Mazungumzo baina ya chama cha Democratic na kile cha Five Star Movement yanajiri baada ya rais Sergio Mattarela kufanya mashauriano ya siku mbili na viongozi wengine wa kisiasa, hatua ambayo ilionekana kuwa mbinu ya kushurutisha vyama hivyo viwili kutafuta mwafaka wa maelewano.

Rais Mattarela anaamini kuwa vyama hivyo viwili vya PD na Nyota tano M5S vinaweza kufanya kazi kwa pamoja licha ya tofauti zao za siasa za hapo awali.

Hata hivyo, iwapo hilo litakosa kufanyika basi Mattarela hatakuwa na budi bali kulivunjilia mbali bunge, hatua ambayo itashurutisha kufanyika kwa uchaguzi wa mapema mwezi Novemba. Pia rais huyo atalazimika kuteua serikali ya mpito ambayo itakua na jukumu la kuandaa uchaguzi huo.

Rais Mattarela anaamini kuwa vyama hivyo viwili vya PD na Nyota tano M5S vinaweza kufanya kazi kwa pamoja licha ya tofauti zao za siasa za hapo awali.
Rais Mattarela anaamini kuwa vyama hivyo viwili vya PD na Nyota tano M5S vinaweza kufanya kazi kwa pamoja licha ya tofauti zao za siasa za hapo awali.Picha: picture-alliance/dpa/ZUMAPRESS/Wire/SOPA Images/C. Martemucci

Vyama hivyo viwili vya M5S na PD vinataka kumuweka kando Salvini ili awe upande wa upinzani, japo kutokana na uhasama baina yao, huenda mazungumzo yao yakagonga mwamba kutokana na sababu mbili kuu, Kwanza kiongozi wa vuguvugu la nyota tano Luigi Di Maio anataka kubakia kwenye wadhifa wa naibu waziri mkuu na pili uamuzi wa muungano huo unafaa kutegemea kura ya mtandaoni itakayopigwa na wanachama wa vuguvugu la nyota tano.

Hata hivyo mfumo huo wa kura za mtandaoni unaojulikana kama Rousseau umeshutumiwa na naibu kiongozi wa chama cha Democratic Andrea Orlando aliyesema kuwa matokeo ya kura hizo yanaweza kuchakachuliwa na wadukuzi.

Salvini ambaye anaongoza chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Liga ndiye aliyechochea mzozo huo wa serikali kwa kuvunja muungano na vuguvugu la Nyota tano M5S uliokuwepo madarakani kwa miezi 14.

Kwa mujibu wa kura za maoni za hivi karibuni, hatua hiyo ya Salvini ya kuvunja muungano na M5S kumechangia kupungua kwa umaarufu wake wa kisiasa.

Uungwaji mkono wa chama chake cha Liga umepungua hadi asilimia 33 kutoka asilimia 36 mwezi uliopita huku vuguvugu la nyota tano likipata uungwaji mkono wa asilimia 19 nacho chama cha PD kikiwa na asilimia 23.