Mzozo wa gaza wazidi kutokota | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mzozo wa gaza wazidi kutokota

Rais Barack Obama wa Marekani amesema nchi yake inaunga mkono hatua ya Israeli kujilinda yenyewe.

Rais Barack Obama na Benjamin Netanyahu

Rais Barack Obama na Benjamin Netanyahu

Matamshi hayo ameyatoa wakati wa mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu yaliyofanyika kwa njia ya simu, kuhusu mgogoro wa Gaza. Rais Obama ameelezea pia masikitiko yake kutokana na vifo vya raia wa Israeli na Palestina. Ikulu ya Marekani imesema kuwa, Netanyahu ambaye alimpigia simu Rais Obama, ametoa shukrani zake kwa Rais Obama na kwa wananchi wa Marekani. Viongozi hao pia wamejadiliana kuhusu kuzuia mzozo huo kusambaa.

Obama azungumza pia na Morsi na Erdogan

Aidha, Rais Obama amempongeza Rais wa Misri, Mohamed Morsi kwa juhudi ya kusaidia kuituliza hali kati ya Israeli na Gaza na kusisitiza matumaini yake ya kurejea kwa utulivu kwenye eneo hilo. Akizungumza na Morsi kwa njia ya simu, Rais Obama ameelezea umuhimu wa kumaliza mashambuliano haraka iwezekanavyo ili kuzuia maisha ya raia wasio ha hatia kupotea bila sababu. Waziri Mkuu wa Misri, Hisham Kandil amesema nchi yake ipo tayari kupatanisha juu ya kusimamisha mashambiliano kati ya Israeli na Hamas. Misri ni mshirika wa Hamas, lakini pia imetiliana saini mkataba wa amani na Israeli mwaka 1979.

Rais wa Misri, Mohammed Morsi

Rais wa Misri, Mohammed Morsi

Mbali na Netanyahu na Rais Morsi, Rais Obama amezungumza pia na Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kwa njia ya simu ambapo kwa pamoja wameelezea wasiwasi wao kuhusu hatari zinazowakabili raia wa pande zote mbili na kuelezea nia yao ya kutaka kumaliza ghasia hizo. Taarifa ya Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Rais Obama na Erdogan pia wamesema ghasia mpya katika Mashariki ya Kati zinahatarisha matarajio ya amani ya kudumu katika eneo hilo.

Mapigano yaendelea

Mazungumzo hayo kwa njia ya simu yamefanyika, wakati wapiganaji wa Hamas wakirusha maroketi kwenye miji ya Jerusalem na Tel Aviv jana Ijumaa. Israeli imesema imezifunga barabara zote kuu kuzunguka mpaka wake na Gaza, na kulielezea eneo hilo kama la kijeshi. Hatua hiyo ni ishara kwamba uvumilivu wa Israeli sasa umefikia kikomo na inajiandaa kuanzisha mashambulizi ya kwanza ya askari wa miguu katika eneo hilo tangu mwaka 2008 na 2009. Kiasi Wapalestina 21 na Waisraeli watatu wameuawa tangu Israeli ilipoanzisha mashambulizi siku ya Jumatano, wakati ilipomuua mkuu wa jeshi la Hamas, Ahmed al-Jabari.

Ban Ki-Moon azitolea wito Israeli na Hamas

Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amezitaka Israeli na Hamas kumaliza mashambulizi yanayoongezeka katika Ukanda wa Gaza ili kuzuia mauaji zaidi katika Israeli na Palestina. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nersiky amesema Ban ana wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa ghasia kati ya Gaza na Israeli na anahofia pia kupanda kwa gharama za maisha ya raia. Nersiky amesema Ban anatarajiwa kuzuru eneo hilo hivi karibuni. Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa Ban atazuru Israeli na Misri wiki ijayo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo
Mhariri: Abdu Mtullya

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com