1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka mmoja wa machafuko nchini Syria

15 Machi 2012

Vuguvugu la maandamano ya umma dhidi ya Rais Bashar al-Assad limedumu kwa muda wa mwaka mmoja tangu lilipoanza. Ulimwengu ungali umegawanyika kuhusu jinsi ya kuumaliza mgogoro huo.

https://p.dw.com/p/14Krb
FILE - In this Sunday, March 11, 2012 file photo, Free Syrian Army fighters celebrate after hearing that their comrades destroyed a Syrian Army tank in Idlib, north Syria. In the previous days, troops had encircled Idlib, and tank shells pounded the city from dawn until evening. Rebels dashed through the streets, taking cover behind the corners of buildings as they clashed with the troops. Wounded fighters were piled into trucks bound for makeshift clinics. (Foto:Rodrigo Abd, File/AP/dapd)
Syrien Bürgerkrieg Kämpfe in Idlib RebellenPicha: AP

Vikosi vitiifu kwa rais Bashar al-Assad vimezishambulia ngome za waasi nchini Syria wiki hii, vikitumia vifaru na makombora mazito kuwashambulia wapinzani mijini na vijijini, ikiwemo mji wa Deraa Kusini mwa nchi hiyo ambako mapinduzi hayo yalianzia mwezi Machi mwaka uliopita.

Huku kukiwa na onyo kuwa Syria inaweza kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu Kofi Annan ameitisha ufafanuzi zaidi kutoka kwa serikali ya Damascus kuhusu jibu la mapendekezo yanayolenga kumaliza machafuko hayo.

Annan kesho Ijumaa anatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloonekana kugawanyika, huku Urusi na China zikizidi kuwa nyuma ya Assad nazo nchi za Magharibi zikishinikiza mabadiliko ya utawala. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takribani watu 8,000 wengi wao raia wameuwawa katika mapigano hayo, huku wengine 230,000 wakitorokea ng'ambo na kuibua hali ya mzozo wa wakimbizi.

al-Assad amesimama kidete

Rais wa Syria alitabiri mwanzoni mwa mwaka 2011 kuwa nchi yake ilikuwa imara dhidi ya kile kilichoitwa “wimbi la megeuzi katika ulimwengu wa Kiarabu” ambalo lilisabaisha viongozi wa muda mrefu nchini Tunisia, Misri, Libya, na Yemen kuondolewa madarakani. Kwa kipindi cha miezi 12, maandamano ambayo yamekuwa ya amani kutaka demokrasia, yamegeuka na kuwa mapinduzi, yakiongozwa na wanagambo wasio kuwa na silaha za kutosha na wanajeshi waasi walioungana kuunda kundi la Jeshi Huru la Syria.

Rais Bashar al-Assad ameitisha uchaguzi wa bunge tarehe 7 Mei
Rais Bashar al-Assad ameitisha uchaguzi wa bunge tarehe 7 MeiPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya uchumi unaosambaratika, vikwazo vinavyoongezeka na kutengwa na jamii ya kimataifa, Assad angali anaonekana kupata uungwaji mkono ndani ya Syria, hasa kutoka miji miwili mikuu Damascus na Aleppo. Mshirika wake mkuu Iran pia angali anamuunga mkono.

Ulimwengu umegawanyika

Hakuna dalili ya familia ya Assad na washirika wake kupoteza udhibiti au kujiuzulu maafisa wakuu kutoka jeshini. Huku mataifa ya Magharibi na yale kutoka Ulimwengu wa Kiarabu yakishtumu ukandamizaji huo wa umwagaji damu, Syria imetegemea uungaji mkono wa Urusi na China ambazo zimepiga kura ya turufu kupinga maazimio mawili ya Umoja wa Mataifa yaliyolaani serikali ya Assad.

Wanadiplomasia hata hivyo wanasema mgogoro huo unaanza kuwa mpasuko wa kimadhehebu, huku kukiwa na Wasunni walio wengi. Wanaojumuisha asilimia 75 ya jumla ya watu milioni 23, na kundi la Alawite lake Assad linalowakilisha asilimia 10 ya wananchi lakini linadhibiti nyadhifa kuu serikalini. Wachambuzi wanasema makundi mengine ya walio wachache kama wakristo wanamuunga mkono Assad kwa hofu ya mashambulizi ya kulipiza kisasi ikiwa ataondolewa madarakani.

Kofi Annan na Rais Bashar al-Assad mjini Damascus
Kofi Annan na Rais Bashar al-Assad mjini DamascusPicha: picture-alliance/dpa

Syria inasema imeijibu miito ya mageuzi na inaitaja katiba mpya iliyoidhinishwa kwenye kura ya maoni mwezi uliopita ambayo iliondoa kipengele kinachompa mamlaka mengi chama tawala cha Assad, Baath. Uchaguzi wa bunge unatarajiwa kuandaliwa Mei 7.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Josephat Charo