1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Museveni azungumza na Zelensky kwa njia ya simu

23 Februari 2023

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefanya mazungumzo ya simu na Rais Volodymyr Zelensky ambaye kwa sasa anazidi kutafuta uungwaji mkono na hasa wa bara la Afrika kupinga uvamizi huo.

https://p.dw.com/p/4NtbB
Großbritannien London 2020 | Yoweri Museveni, Präsident Uganda
Picha: Henry Nicholls/REUTERS

Uganda ni mojawapo ya mataifa yaliyojizuia  kupiga kura ya kuishtumu na kuilaani  Urusi kwa vita hivyo kwenye kikao cha Umoja Mataifa mwaka uliopita, jambo ambalo liilibua mjadala ndani na nje ya nchi hiyo.

Soma pia: Guterres alaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka jana uliitumbukiza dunia katika mtikisiko mkubwa wa kiuchumi na kisiasa na wakati vita hivyo vikitimiza mwaka kesho, dunia imeanza kufanya tathmini kuhusu hali ya vita hivyo na madhara yake kwa nchi za ulimwengu. Rais Zelensky amezungumza na rais wa Uganda Yoweri Museveni na hatua yake hiyo imeleta mitizamo mbali mbali na hasa kwakuwa Uganda ni moja kati ya mataifa yaliyoonesha msimamo wa kujizuia kushiriki kura ya kuishtumu Urusi kwa uvamizi huo.

Athari za vita vya Ukraine kwa watumiaji wa ngano Afrika

Msimamo huo wa serikali ya Kampala umekuwa ukitazamwa kama ishara inayoonesha kuiunga mkono Urusi na uvamizi wake  huo kama zinavyotazamwa pia nchi kama China na India ambazo pia hazikushiriki kura hiyo. Kwenye ujumbe wake wa twitter, rais Museveni amefahamisha kuwa mazungumzo kati yao yalihusiana na masuala kati ya mataifa hayo  mawili. Lakini watu mbalimbali nchini Uganda wanahisi  haiwezekani rais Zelensky kukosa kuligusia suala la vita kati  nchi yake na Urusi katika mazungumzo hayo.

Na baadhi ya raia wa Uganda kama ilivyo kwa mataifa mengine, wanaamini - kuna haja ya suluhu kupatikana kwa njia ya kidiplomasia  kumaliza vita hivyo ambavyo vimekuwa na athari kubwa kwao

Wakati Urusi ikivamia Ukraine, wachambuzi masuala ya kisiasa wamekuwa wakitowa maoni mbali mbali kuhusu dhamira ya Urusi juu ya uvamizi wake Ukraiune na mwelekeo mzima wa vita hivyo.  Pamoja na hayo katika miezi kumi na mbili, vita vinaendelea huku athari zake kwa uchumi wa dunia zikiendelea kushuhudiwa. 

Ikumbukwe kuwa rais Museveni anaelekea kutawazwa kuwa mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano wa mataifa yasiyofungamana na upande wowote. Kwa hali hiyo, rais Zelensky anamtarajia yeye kama mwanasiasa maarufu barani kuyashawishi mataifa ya afrika ambayo pia hayakushiriki katika kuishtumu Urusi yabadili msimamo wao. Mataifa hayo ni pamoja na Burundi, Senegal, Sudan Kusini,  Africa kusini , Mali and Msumbiji. Kenya, Ghana, Gabon, Rwanda, Djibouti, Congo, Somalia na Jamhuri ya kidemokrasia ya congo yaliunga mkono kura hiyo ya shtuma dhidi ya urusi.

Lubega Emmanuel DW Kampala